Pata taarifa kuu

Polisi ya Italia yakanusha madai ya Amnesty kuhusu visa vya mateso kwa wahamiaji

Siku moja baada ya shirika la kimataifa la haki za binadamu la Amnesty Inetrnational kushtumu polisi ya italia kuwafanyia mateso wahamiaji waishio katika makambi mbali mbali nchini Italia, mkuu wa polisi ya nchi hiyo amekanusha shutma hizo.

Wahamiaji wakiwasili kwa meli ya kijeshi ya Italia katika bandari ya Naples. Tarehe 6 Mei 2015.
Wahamiaji wakiwasili kwa meli ya kijeshi ya Italia katika bandari ya Naples. Tarehe 6 Mei 2015. AFP PHOTO / MARIO LAPORTA
Matangazo ya kibiashara

"Napinga madai yanayosema kwamba kulitumiwa mbinu za kikatili dhidi ya wahamiaji, katika zoezi la kuwatambua na kuwarejesha katika nchi walikotokea," amesema katika taarifa yake Alhamisi hii mkuu wa polisi ya Italia, Franco Gabrielli.

Shirika la kimataifa la haki za binadamu, Amnesty International limesema polisi wa Italia wanawapiga na kutumia vifaa vya umeme wahamiaji katika mchakato wa kuchukua alama za vidole.

Ripoti ya shirika hilo inasema shinikizo la Umoja wa Ulaya kwa Italia katika kuwashughulikia wakimbizi na wahamiaji limesababisha wakimbizi na wahamiaji kufukuzwa kinyume cha sheria pamoja na ukatili dhidi ya wakimbizi ambapo katika baadhi ya kesi inaweza kuwa ni mateso.

Mchakato wa kuchukua alama za vidole unalenga kuwazuia wahamiaji kutoweza omba tena hifadhi katika mataifa mengine lakini kwa mujibu wa ushuhuda uliotolewa na wahamiaji karibu 170 kumekuwa na unyanyasaji hata kwa watoto wadogo. Baadhi ya wahamiaji hawataki kuchukuliwa alama za vidole kwa matumaini ya kuendelea na safari katika mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya na kuomba hifadhi.

Kwa mwaka jana pekee Ulaya ilishuhudia wimbi kubwa la wakimbizi na waomba hifadhi zaidi ya milioni moja ambao wanakimbia vita na umaskini katika mgogoro mbaya kushuhudiwa tangu vita vya pili vya dunia.

Mtafiti wa shirika hilo kwa Italia Matteo de Bellis amesema "Wahamiaji wengi wanakataa kuchukuliwa alama za vidole kwa sababu wanataka kwenda katika mataifa mengine ya Ulaya ambako wanadhani huenda wakakutana na ndugu zao. Lakini wanapokataa, maafisa wa Italia wanatumia nguvu dhidi yao. Na tumepokea ushuhuda wa watu ambao wametuambia kuwa wamepigwa, makofi na mateke na polisi wa Italia" amesema mtafiti huyo.

Matteo de Bellis amesema vitendo hivyo vinaleta hofu kwa wakimbizi ambao huwasili Italia badaa ya safari ndefu na ya tabu na wakati mwingine kunyanyaswa wakiwa mikononi mwa polisi na kufukuzwa kinyume na sheria.

Katika kesi 26 za unyanyasaji ambazo Amnesty International imezirekodi, 16 zinahusisha upigwaji na katika kesi karibu zote watu wamesema pia walipigwa na vifaa vya umeme akiwepo kijana wa miaka 16 kutoka Sudan.

"Walinipiga na fimbo ya umeme mara nyingi katika mguu wangu wa kushoto na kisha kulia, kifuani na tumboni. Niliishiwa nguvu, sikuweza kupinga na katika hatua hiyo walichukua mikono yangu na kuifunga katika mshine, " kijana huyo kutoka Sudan amesema.

"Tunachoweza kusema ni kwamba tumepokea kesi 24 za watu waliotuambia kuwa wametendwa vibaya. Katika mtazamo wetu, tunaona hii ni idadi kubwa na ni muhimu kwa mamlaka za Italia kutazama nini kinaendelea na kulitatua tatizo, " amesema Bw Matteo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.