Pata taarifa kuu
MYANMAR-UINGEREZA

Waziri Mkuu wa Uingereza kuzuru Myanmar mwishoni mwa juma hili

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron anatarajiwa kuzuru nchini Myanmar baadaye juma hili na atakuwa Kiongozi wa kwanza wa juu kutoka Mataifa ya Magharibi kutembelea taifa hilo ambalo limeongozwa kwa Utawala wa Kijeshi kwa miongo kadhaa kabla ya kusitishwa hapo mwaka jana.

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron anayetarajiwa kuzuru nchini Myanmar hapa akizungumza na Wanahabari huko Ubelgiji, Brussels
Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron anayetarajiwa kuzuru nchini Myanmar hapa akizungumza na Wanahabari huko Ubelgiji, Brussels REUTERS/Francois Lenoir/Files
Matangazo ya kibiashara

Serikali ya Myanmar imethibitisha uwepo wa ziara hiyo ya Waziri Mkuu Cameron ambaye anatarajiwa pia kukutana na Rais Thein Sein kwa mazungumzo ambayo yatafanyika katika Mji Mkuu Naypyidaw kabla ya kukutana na Kiongozi wa Upinzani na Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Aung San Suu Kyi.

Afisa wa Serikali ya Myanmar amesema kuwa ziara hiyo ya Waziri Mkuu Cameron itakuwa ni ya siku moja ambapo atakutana na Suu Kyi huko Yangon kabla ya kuondoka na kurejea London baada ya mazungumzo hayo.

Miongoni mwa vitu ambavyo vinatajwa vitajadiliwa baina ya Waziri Mkuu Cameron na viongozi hao wa Myanmar ni pamoja na suala la demokrasia pamoja na kulegeza vikwazo kwa nchi hiyo inayotekeleza juhudi za kusimika demokrasia.

Mmoja wa watu waliokaribu na Suu Kyi amesema kuwa Waziri Mkuu Cameron atarakutana na Mshindi huyo wa Tuzo ya Amani ya Nobel siku ya ijumaa kitu ambacho kinadhihirisha huenda ziara hiyo ikafanyika mwishoni mwa juma hili.

Ziara ya Waziri Mkuu Cameron inakuja wakati ambapo Suu Kyi akitarajiwa kuingia Bungeni kwa mara ya kwanza tarehe ishirini na tatu ya mwezi huu kufuatia ushindi ambao aliupata kwenye kinyang'anyiro cha ubunge kilichofanyika mapema mwezi huu.

Suu Kyi ambaye alikuwa kwenye kifungo cha miaka kumi na tano kati ya miaka ishirini na mbili iliyopita amekuwa mstari wa mbili kumsihi Rais Sein kuendelea kuhakikisha mabadiliko yanachukua nafasi katika nchi hiyo.

Marekani imekuwa nchi ya kwanza kutangaza uamuzi wake wa kulegeza vikwazo ambavyo ilikuwa imeviweka dhidi ya nchi ya Myanmar kitu ambacho kinaweza kutoa ahueni kwa taifa hilo.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.