Jeshi la Israeli laendeleza mashambulio kwenye mji wa Rafah, Gaza
Nairobi – Jeshi la Israeli limeendeleza mashambulio ya angaa dhidi ya kundi la Hamas kwenye mji wa Rafah huko Gaza, wakati huu likijiandaa kuanza operesheni ya ardhini kwenye mji huo.
Imechapishwa:
Viongozi wa Hamas kwenye ukanda wa Gaza wanaonya kuwa mpango huo wa jeshi la Israeli, utasababisha mauaji na majeraha makubwa kwa raia wa kawada kwenye eneo hilo la Rafah, lenye watu wengi.
Siku ya Ijumaa, Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu, aliwaambia Mawaziri kuwasilisha mpango wa kuwaondoa wananchi kwenye mji huo kabla ya kutumwa kwa vikosi vya ardhini.
Mpango huu umelaaniwa na rais wa mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas, ambaye amesema hatua ya Israeli inatishia usalama na amani ya kikanda na inavuka mstari mwekundu.
Saudi Arabia nayo imeonya kuwa iwapo Israeli itaendelea na mpango wake, itababisha janga kubwa la binadamu katika ukanda wa Gaza na kulitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuingilia kati.
Tangu kuanza kwa vita kati ya Jeshi la Israeli na kundi la Hamas tangu Oktoba 7 mwaka uliopita, watu wanaokadiriwa kuwa 1,160 wameuawa nchini Israeli na wengine karibu elfu 28 wakiuawa kwenye ukanda wa Gaza.