ICJ kutoa uamuzi kuhusu madai ya Israel kutekeleza mauaji ya kimbari Gaza
Nairobi – Majaji wa Mahakama ya kimataifa ya haki ICJ, leo watatoa uamuzi wao wa awali kuhusu kesi iliyowasilishwa na Afrika Kusini, ikiishtaki Israeli kwa kutekeleza mauaji ya kimbari kwenye ukanda wa Gaza.
Imechapishwa:
Cheza - 01:07
Mahakama hiyo haitarajiwi kutoa hukumu dhidi ya Israeli na kuamua iwapo jeshi lake linatekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya raia wa Palestina kwenye ukanda wa Gaza au la.
Kinachotarajiwa kutokea ni kuwa, huenda Majaji hao wakaimbia Israeli kuachana na operesheni zake za kijeshi kwenye eneo la Gaza, ambazo zimekuwa zikiendelea tangu Oktoba 7 mwaka uliopita, au kuruhusu misaada ya binadamu kuwafikia wanaothiriwa na vita hivyo.
Ripoti zinasema kuwa, katika hatua hii, Majaji watatoa maelekezo kuhusu kesi hiyo, kabla ya baadaye kutoa mtazamo wake kuhusu iwapo, mauaji ya kimbari yanatokea kwenye ukanda wa Gaza, mchakato ambao unaelezwa utachukua miaka.
Katika kesi hiyo, Afrika Kusini inaishtumu Israeli kwa kukiuka kifungu cha mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 1948, dhidi ya mauaji ya halaiki.
Hata hivyo, Israeli imekanusha madai ya Afrika Kusini, kwa kile inachosema kuwa nchi hiyo imekosa hoja na haielewi kinachotokea, na ilichofanya ni kupotosha ukweli wa operesheni yake kwenye ukanda wa Gaza.