Mlipuko Beirut: Rais wa Lebanon afutilia mbali uchunguzi wa kimataifa
Rais wa Lebanon Michel Aoun, ametupilia mbali uchunguzi wowote wa kimataifa kuhusu mlipuko mbaya uliyotokea katika bandari ya mjini Beirut, ambao uligharimu maisha ya zaidi ya watu 150, akibaini kwamba uchunguzi huo utapotosha ukweli.
Imechapishwa:
Rais wa Lebanon pia amesema ni muhimu kurejelea upya mfumo wa kisiasa "uliozorota", siku moja baada ya mwenzake wa Ufaransa, Emmanuel Macron, kuzuru nchi hiyo na kutoa wito kwa viongozi "kubadili mfumo" wa kisiasa nchini Lebanon.
"Tunatakiwa kurejelea upya mfumo wetu wa makubaliano, kwa sababu umezorota na hauruhusu kuchukuwa maamuzi ambayo yanaweza kutekelezwa kwa haraka: lazima kukubaliana na kupitia mamlaka kadhaa," rais Aoun amesema.
Siku ya Alhamisi waandamanaji wenye hasira walikabiliana na maafisa wa usalama jijini Beirut wakilaani mlipuko uliotokea katika ghala la kuhifadhi kemikali.
Waandamanaji wanailaumu serikali kwa utepetevu, suala ambalo wanaamini lilisabababisha mlipuko huo mkubwa na sasa wanataka uchunguzi wa kimataifa kufanyika.