Ufaransa yasema waasi wa Islamic State wataondolewa kabisa mjini Raqa
Muungano wa nchi za Magharibi unaopambana na kundi la Islamic State nchini Syria, unasema hivi karibuni wapiganaji hao wataondolewa kabisa kutoka katika ngome yao kuu ya mji wa Raqa.
Imechapishwa:
Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian amesema jeshi la muungano wa nchi hizo lipo tayari kwa makabiliano hayo.
"Leo, tunaweza kusema kuwa mji wa Raqa utashuhudia makabiliano makali hivi karibu,” amekiambia kituo cha Televisheni cha CNEWS.
Mji wa Raqa umekuwa ngome ya muda mrefu wa kundi la Islamic State nchini Syria pamoja na ile wa Mosul nchini Iraq.
Hata hivyo, Le Drian amesema makabiliano hayo yatakuwa magumu lakini ni lazima wapiganaji hao wakabiliwe.
Kundi la Islamic State nchini Syria pia limekuwa likishambuliwa na wanajeshi wa Urusi, nchi ambayo kwa sasa ni mshirika wa karibu wa rais Bashar Al Assad.
Wakati hayo yakijiri, mazungumzo ya amani kuhusu mzozo wa Syria yanaendelea jijini Geneva nchini Uswizi kati ya serikali ya Damascus na upinzani.
Mazungumzo haya yanaongozwa na Msuluhishi wa Umoja wa Mataifa Staffan de Mistura.