Pata taarifa kuu
SAUDI ARABIA-USALAMA

Viongozi wa Saudi Arabia waahidi kuanzisha uchunguzi wa haraka

Viongozi wa Saudi Arabia wameahidi kuanzisha uchunguzi wa "haraka uliyo wazi" baada ya Mahujaji kukanyagana na kusababisha maafa makubwa. Zaidi ya Mahujaji 700 wamefariki Alhamisi wiki hii katika mji wa Mina karibu na mji mtakatifu wa Makkah wakati wa ibada ya Hijja, ambayo ni nguzo ya tano ya Uislam.

Miili ya Mahujajiwaliofariki wakiwa katika ibada ya Hijja, mjini Mina karibu na mji mtakatifu wa Makkah baada ya kukanyagana, Septemba 24, 2015.
Miili ya Mahujajiwaliofariki wakiwa katika ibada ya Hijja, mjini Mina karibu na mji mtakatifu wa Makkah baada ya kukanyagana, Septemba 24, 2015. STR/AFP
Matangazo ya kibiashara

Hili ni janga kuwahi kutokea katika ibada ya Hijja tangu miaka 25 iliyopita nchini Saudi Arabia ambapo mahujaji milioni mbili wamekusanyika mwaka huu.

Mfalme Salman wa Saudi Arabia ametoa agizo la kupitiwa upya kwa masuala ya hija baada ya watu zaidi mia saba kufariki kutokana msongamano nje ya msikiti wa Makkah.

Idara ya ulinzi wa raia nchini humo imesema watu wengine 863 wamejeruhiwa katika kisa hicho kilichotokea eneo la Mina, takriban kilomita tano kutoka mji mtakatifu wa Makkah.

Maafa hayo yalitokea mahujaji takriban milioni mbili walipokuwa wakishiriki moja ya kaida muhimu za mwisho katika ibada za Hijja.

Mahujaji husafiri hadi Mina wakati wa kuhiji kurusha mawe saba kwenye nguzo saba zijulikanazo kama Jamarat, ambazo huwakilisha shetani.

Nguzo hizo zimo katika eneo ambalo inaaminika kuwa Nabii Ibrahim alijaribiwa na shetani.

Watu walikuwa wakielekea eneo la kurushia mawe, na wengine wakitokea huko pale ghafla watu walipoanza kuanguka.

Idara ya ulinzi wa raia Saudi Arabia imesema mkanyagano huo ulitokea pale kulipotokea "ongezeko la ghafla" la watu waliokuwa wakielekea kwenye kwenye nguzo za kurushiwa mawe.

Waziri wa afya wa Saudi Arabia Khaled al-Falih amesema mkanyagano huo ulitokea kwa sababu mahujaji walikosa kufuata maagizo.

Mkanyagano huo umetokea siku ya kwanza ya sherehe za Eid al-Adha.
Wizara ya usalama wa raia ya Saudi Arabia imesema maafisa 4,000 wametumwa eneo hilo kusaidia pamoja na wahudumu 200 wa huduma za dharura.

Maandalizi ya ibada hizo za Hija yalikuwa yamekumbwa na mkasa baada ya kreni kuanguka katika msikiti mkuu wa Makkah mwezi huu na kuua watu 109.
Hii si mara ya kwanza kwa mikasa kutokea wakati wa Hijja.

Mikasa mingine iliyotokea wakati wa kuhiji:

2006: Mahujaji 364 walifariki wakati wa kurushia mawe mnara unaoashiria shetani unaojulikana kama Jamarat.

1997: Mahujaji 343 walifariki na 1,500 kujeruhiwa kwenye mkasa wa moto

1994: 270 waliuawa katika mkanyagano

1990: Mahujaji 1,426 waliuawa katika mkanyagano njia za kupitia chini za kuelekea maeneo matakatifu

1987: Watu 400 walifariki maafisa wa serikali walipokabiliana na waandamanaji waliounga mkono Iran.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.