Pata taarifa kuu
SYRIA

Nchi ya Syria yatia saini makubaliano kuruhusu waangalizi wa kimataifa kuingia nchini humo

Serikali ya Syria kupitia kwa waziri wake wa mambo ya nje Walid Muallem ametangaza nchi yake kutia saini makubaliano ya kuruhusu waangalizi wa kimataifa toka nchi wanachama wa Umoja wa Kiarabu kuingia nchini humo kuchunguza tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu na vikosi vya usalama. 

Waziri wa mambo ya nje wa Syria Walid Muallem
Waziri wa mambo ya nje wa Syria Walid Muallem Reuters
Matangazo ya kibiashara

Katika makubaliano hayo mapya kati ya Syria na Umoja wa nchi za Kiarabu yanakuja wakati ambapo awali Umoja huo ulitishia kuifutia uanachama nchi ya Syria kutokana na Serikali kuendelea kukaidi maagizo ya kusitisha machafuko nchini mwake.

Mkataba huo mpya ambao umesainiwa na ujumbe maalumu wa viongozi wa Syria nchini Qatar Doha unaitaka nchi hiyo kuruhusu waangalizi wa kimataifa wa haki za bindamu kuingia nchini humo kwa muda wa mwezi mmoja pekee kama ilivyokubaliwa.

Awali nchi ya Syria ilikataa kutia saini makubaliano hayo baada ya Umoja huo kutaka waangalizi hao kukaa nchini humo kwa zaidi ya miezi miwili kwa kile ilichodai kuwa hatua hiyo huenda ingeendelea kuchochea machafuko zaidi.

Katika makubaliano hayo pia nchi ya Syria imeruhusu waangalizi toka nchi za kiarabu pekee.

Akiongea katika mkutano wake na waandishi wa habari, waziri huyo ameongeza kuwa nchi yake haipaswi kulaumiwa kwa kile ambacho kinatokea nchini humo kwakuwa matukio mengi yanachochewa na mataifa ya magharibi.

Muallem pia amekanusha nchi yake kusaini makubaliano hayo kwakuwa ilitishiwa kupelekwa katika kikao cha Baraza la Usalama la umoja wa Mataifa hatua ambayo pengine ingeshuhudia nchi hiyo ikivamiwa kijeshi.

Nchi ya Syria imekuwa ikilaumiwa na jumuiya ya Kimataifa kwa kukataa kwake kuruhusu waangalizi wa Kimataifa kuingia nchini humo hatua iliyofanya makubaliano haya kuchukua muda kuafikiwa.

Mbali na kutia saini makubaliano hayo, pia waziri Muallem amesema kuwa nchi yake inaendelea na mazungumzo na viongozi wa Umoja wa Kirabu kuangalia uwezekano wa kupata suluhu ya kudumu na viongozi wa upinzani ambao wamekuwa wakihamasisha maandamano kupinga utawala wa rais Bashar al-Asad.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.