Pata taarifa kuu
UN-AU-ICC-KENYA

Wajumbe wa UNSC kupiga kura Ijumaa hii kuamua hatma ya kesi za Kenya kwenye mahakama ya ICC

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN, linatarajiwa kupiga kura Ijumaa ya wiki hii kuamua kuhusu ombi la nchi za Umoja wa Afrika AU kutaka mahakama ya kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ICC kuahirisha kesi dhidi ya viongozi wa Kenya kwa mwaka mmoja zaidi.

Mwendhesha mashtaka mkuu wa mahakama ya ICC, Fatou Bensouda akiwa kwenye moja ya vikao vya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, UN
Mwendhesha mashtaka mkuu wa mahakama ya ICC, Fatou Bensouda akiwa kwenye moja ya vikao vya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, UN UN
Matangazo ya kibiashara

Majuma kadhaa yaliyopita viongozi wa Umoja wa Afrika waliwasilisha ombi maalumu kwenye baraza la usalama la Umoja huo wakitaka kesi dhidi ya rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto ziahirishwe kwa mwaka mmoja kuwapa nafasi kuongoza vema nchi yao.

Ombi la Umoja wa Afrika limeletwa kufuatia madai ya Serikali ya Kenya kuwa nchi yao haiko vizuri kiusalama hasa wakati viongozi wake wanahudhuria vikao vya kesi zao mjini The Hague na kwamba kutokuwepo kwao kutawapa nafasi magaidi kutekeleza matukio zaidi.

Tayari baadhi ya nchi wanachama wa Umoja wa Afrika wameunga mkono nchi zao kujiondoa kwenye mkataba wa Roma jambo ambalo hata hivyo licha ya kujadiliwa mara kadhaa nchi nyingi haziungi mkono kujiondoa kwenye mkataba huo.

Uganda imekuwa mstari wa mbele kuyashawishi mataifa mengine kujiondoa kwenye mkataba wa Roma huku wabunge nchini Kenya wenyewe wakipitisha azimio la kuanza mchakato wa kujiondoa kwenye mkataba unaotambua mahakama ya ICC.

Balozi wa Rwanda kwenye Umoja wa Mataifa, Eugene Richard Gasana amewaambia waandishi wa habari mjini New York kuwa wajumbe wa baraza la usalama wamekuwa wakijadili ombi la Umoja huo na kwamba huenda wakapiga kura kukubaliana na kuahirisha kesi hizo kwa mwaka mmoja.

Baadhi ya mataifa ya Umoja wa Ulaya EU yameshaweka wazi msimamo wao wakutounga mkono pendekezo hili la Umoja wa Afrika wakiamini kuwa halitapitishwa kwakuwa mswada wao haukuwa na hoja za msingi kufanya kesi hizo kuahirishwa.

Rais Kenyatta na naibu wake William Ruto wanashtakiwa kwenye mahakama ya ICC kwa tuhuma za kuhusika na makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu wakati wa machafuko ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 ambapo watu zaidi ya elfu moja walipoteza maisha.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.