Pata taarifa kuu
SYRIA

Umoja wa Mataifa waamua kuwaondoa waangalizi wake nchini Syria

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwaondoa waangalizi wake nchini Syria kufikia siku ya Jumapili.

Matangazo ya kibiashara

Uamuzi huo uliafikiwa katika mkutano wa wajumbe hao mjini New York nchini Marekani siku ya Alhamisi baada ya wajumbe hao kusema kuwa malengo ya waangalizi hao hayakutimia wala kutekelezwa.

Akitoa tangazo hilo Balozi wa Ufaransa katika Umoja huo Gerard Araud alisema kufikia Jumapili usiku, shughuli za waangalizi hao zitafikia tamati na wataondoka nchini Syria.

Mapema mwaka huu, Umoja wa Mataifa ulituma waangalizi 300 wa kijeshi nchini humo kufuatilia utekelezwaji wa mpango wa aliyekuwa msuluhishi wa mzozo huo Koffi Annan uliolenga kumaliza machafuko hayo ambayo yamedumu kwa miezi 17 sasa na kusababisha maelfu ya watu kuuawa na wengine kutoroka makwao.

Katika hatua nyingine, machafuko zaidi yameendelea kuripotiwa katika mji wa Alllepo ambapo wanajeshi wa serikali wanatumia ndege za kivita kuwalenga wapiganaji wa upinzani.

Wanarahakati wa haki za binadamu nchini humo wanasema zaidi ya watu mia moja waliuliwa siku ya Alhamisi katika mji huo hasa katika eneo la Azaz.

Mashirika hayo yanataka baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio la kuiwekea Syria vikwazo vya silaha jambo ambalo huenda lisifanyike kutokana na Urusi na Uchina kuendelea kutumia kura zao za veto kupinga azimio lolote dhidi ya serikali ya rais Bashar Al Assad.

Mkurungezi Mkuu wa maswala ya kibinadamu katika Umoja wa Mataifa Valerie Amos aliyezuru Damascus mapema wiki hii alisema hali ya kibinadamu ni mbaya sana nchini humo na zaidi ya watu Milioni 2 wanahitaji misaada ya haraka ya kibinadamu hasa chakula, makaazi na huduma za matibabu.

 

 

 

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.