Pata taarifa kuu
KENYA-UCHAGUZI

Kura zaanza kupigwa Nchini Kenya

Wakenya zaidi ya Milioni 19, wanatarajiwa kushiriki katika Uchaguzi Mkuu kutoka Kaunti zote 47 nchini Kenya na mbali na urais, watachaguwa Magavana, Maseneta, Wabunge, Wawakilishi wa Wanawake na wawakilishi wa serikali za Kaunti.

Wakenya wapiga kura mjini Mombasa
Wakenya wapiga kura mjini Mombasa Joseph Jira/RFI Mombasa
Matangazo ya kibiashara

Zoezi la upigaji kura limeanza katika maeneo mbalimbali nchini Kenya katika uchaguzi mkuu huu. Raia 19m wamejiandikisha kupiga kura.

Wagombea wanaowania kinyang'anyiro cha urais ni wanane, lakini ushindani mkubwa ni kati ya Rais anayemaliza muda wake Uhuru Kenyatta na mpinzani mkuu Raila Odinga.

Bw Odinga anawania urais kwa mara ya nne.

Vituo vya kupigia kura vitafungwa saa kumi na moja jioni. Kuna jumla ya vituo 40,883 vya kupigia kura kote nchini

Wakenya wapiga kura mjini Mombasa
Wakenya wapiga kura mjini Mombasa Joseph Jira/RFI Mombasa

Siku ya Jumatatu, Tume ya Uchaguzi nchini Kenya ilisema iko tayari kusimamia Uchaguzi Mkuu unaofanyika leo Jumanne Agosti 8.

Maafisa wa Tume ya Uchaguzi walipokea vifaa vya kupigia kura, ikiwemo masanduku na karatasi za kupigia kura.

Kampeni zilimalizika  Jumamosi iliyopita huku ushindani mkubwa wa urais ukiwa ni kati ya rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga. Wote wamesema wana imani kuwa watashinda Uchaguzi huu.

Rais Kenyatta atapiga kura katika eneo la bunge la Gatundu katika Kaunti ya Kiambu, huku Odinga akipiga kura yake katika Shule ya Msingi ya Olympics, katika mtaa wa Kibera jijini Nairobi.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Wafula Chebukati, amewahakikishia Wakenya kuwa wao kama Tume wameweka mikakati yote tayari kuhakikisha kuwa zoezi hili linakwenda vizuri na Uchaguzi unakuwa huru na haki.

Aidha, amesema kuwa Wakenya wasiwe na wasiwasi  kuhusu urushaji na kutangazwa kwa matokeo kwa sababu ni suala ambalo limeshughulikiwa ipasavyo.

Kumekuwa na Wakenya wengi wanaosafiri vijijini, kwa kile wanachosema wanakwenda kupiga kura.

Hata hivyo, kumekuwa na mashaka kuwa wengine wamerudi vijijini kwa sababu wanahofia kuwa huenda kukazuka machafuko kama ilivyokuwa baada ya Uchaguzi wa mwaka 2007.

Wito umekuwa ukitolewa kwa wananchi wa taifa hilo, kudumisha amani kabla na baada ya uchaguzi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.