Pata taarifa kuu
ULINZI-DIPLOMASIA

Jeshi la Afrika Mashariki nchini DRC: Uganda kupeleka wanajeshi elfu moja

Uganda imetangaza siku ya Jumanne kwamba itatuma wanajeshi elfu moja ifikapo mwishoni mwa mwezi Novemba mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kama sehemu ya kikosi cha kanda ya Afrika Mashariki kilichotumwa katika eneo hili linalokabiliwa na makundi yenye silaha.

Moja ya operesheni ya pamoja kati ya majeshi ya Uganda na DRC katika Hifadhi ya Taifa ya Virunga nchini DRC, Desemba 14, 2021.
Moja ya operesheni ya pamoja kati ya majeshi ya Uganda na DRC katika Hifadhi ya Taifa ya Virunga nchini DRC, Desemba 14, 2021. © SEBASTIEN KITSA MUSAYI/AFP
Matangazo ya kibiashara

"Tunakamilisha maandalizi ya wanajeshi wetu kabla ya kuwatuma mashariki mwa DRC" pamoja na wanajeshi wa Kenya ambao tayari wako mjini Goma, msemaji wa jeshi la Uganda Felix Kulayigye ameliambia shirika la habari la AFP. "Tunatuma karibu akari 1,000," amesema, bila kutoa tarehe kamili ya kuondoka.

Vyanzo viwili vya kijeshi vimeliambia shirika la habari la AFP kwamba timu za kijasusi, matibabu na vifaa tayari ziko Goma kujiandaa na mpango wa kutumwa kwa wanajeshi hawa 1,000, chini ya tishio la mashambulizi ya M23, waasi wa zamani wa Kitutsi ambao walichukua silaha tena mwishoni mwa 2021.

Nchi saba za Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki (EAC) - Burundi, Kenya, Uganda, DRC, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania - ziliamua mwezi Juni kutuma jeshi la kikanda ili kuleta utulivu mashariki mwa DRC, eneo linalokumbwa na ghasia kwa karibu miaka 30.

Mashambulizi ya hivi majuzi ya M23 yamechochea mvutano wa kidiplomasia kati ya DRC na Rwanda.

Kinshasa inaishutumu Rwanda kwa kutoa msaada kwa kundi la waasi wa M23 ambao wataalamu wa Umoja wa Mataifa na maafisa wa Marekani pia walieleza katika miezi ya hivi karibuni. Kigali inapinga, ikiishutumu Kinshasa kwa kushirikiana na FDLR, waasi wa Kihutu wa Rwanda kundi, lililoanzishwa nchini DR Congo tangu mauaji ya halaiki ya Watutsi mwaka 1994 nchini Rwanda.

Kenya inaongoza ujumbe wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, unaojumuisha pia wanajeshi kutoka Burundi na Sudan Kusini.

Wanajeshi wa Kenya na Uganda watatumwa pamoja na wanajeshi wa Kongo katika mkoa wa Kivu Kaskazini na Ituri, jeshi la Sudan huko Haut-Uélé na Warundi katika mkoa wa Kivu Kusini. Kikosi cha wanajeshi wa Rwanda kitatumwa kwenye mpaka, baada ya Kinshasa kupinga ushiriki wa Kigali katika operesheni yoyote katika ardhi yake.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.