Pata taarifa kuu
UMOJA WA ULAYA EU

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakutana kwa dharura jijini Brussels kuijadili Urusi

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakutana Alhamisi hii katika kikao cha dharura mjini Brussels nchini Ubelgiji kuamua hatua za kuichukulia Urusi, baada ya kutuma jeshi lake katika eneo la Crimea nchini Ukraine.

Matangazo ya kibiashara

Baadhi ya viongozi wa Umoja huo kutoka Mashariki mwa Ulaya wanataka serikali ya rais Vladimir Putin kuwekewa vikwazo vya kiuchumi na siasa lakini Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anaona ni vema ikiwa mazungumzo yatatumiwa kuipatanisha Urusi na Ukraine.

Katika hatua nyingine, rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso amesema kuwa Umoja huo utatoa msaada wa Dola Bilioni 15 kwa serikali ya Ukraine ili kujikwamua Kiuchumi baada ya uchumi wake kuanza kudorora kutokana na mzozo wa kisiasa na usalama unaendelea nchini humo.

Wakati uo huo, Katibu Mkuu wa Majeshi ya nchi za kujihami NATO Anders Fogh Rasmussen amesema kuwa jeshi hilo linaangalia upya uhusiano wake na Urusi katika juhudi zinazofanyika kuishinikiza serikali ya Urusi kuyaondoa majeshi yake nchini Ukraine.

Haya yote yanajiri baada ya wawakilishi wa Marekani na Urusi kukutana jijini Paris nchini Ufaransa siku ya Jumatano na kuahidi kuendelea kuzungumza kuhusu hali ya usalama na kisiasa nchini Ukraine.

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry na mwenzanke wa Urusi wa Sergei Larvov wamesema mazungumzo yao hayakuwa mepesi lakini hawana lingine bali kuendelea kuzungumza kupata suluhu la kudumu.

Katika mkutano huo Lavrov alikataa kukutana na Waziri wa Mambo ya nje wa Ukraine Andriy Deshchytsia, kwa sababu Moscow haiitambui serikali iliyoko madarakani na juhudi za Kerry kujaribu kumshawishi Larvov kukutana na mwakilishi huyo wa Ukraine ziliambulia patupu.

Urusi imeendelea kushtumiwa kuivamia Ukraine kijeshi tuhma ambazo Moscow inakanusha kwa kile inachokisema kuwa ilikwenda kuisaidia nchi hiyo baada ya ombi kutoka kwa rais wa zamani Viktor Yanukyovich na pia walikwenda kuwalinda raia na maslahi yao katika eneo hilo la Crimea.

Brian Wanyama ni mchambuzi wa siasa za Kimaifa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Masinde Muliro nchini Kenya ameimbia RFI Kiswahili kuwa Jumuiya ya Kimataifa itafanikiwa kusuluhisha mgogoro huu kwa kuileta Urusi na Ukraine katika meza ya mazungumzo.

Marekani pamoja na Mataifa mengine ya Magharibi yamesema yatasimama na Ukraine na kuipa msaada wa kifedha na kijeshi.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.