Pata taarifa kuu
UFARANSA-AFRIKA

Ufaransa yapongezwa kwa kuwatuma wanajeshi wake katika maeneo yenye migogoro barani Afrika

Aliyekuwa zamani katibu mkuu wa Umoja wa mataifa UN, Kofi Annan, ameipongeza serikali ya Ufaransa kujituma katika kusuluhisha migogoro ya kivita inayoendelea kujienea barani Afrika. Akiwa ziarani jijini Paris nchini Ufaransa, Anan amesema kitendo cha Ufaransa kuwatuma wanajeshi wake nchini Mali lakini pia nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati ni mfano unaofaa kuigwa na mataifa mengine duniani.

REUTERS/Stringer
Matangazo ya kibiashara

Kauli ya Annan inakuja wakati huu ambapo Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian akiwasili nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kufanya mazungumzo na viongozi wa serikali ya mpito.

Le Drian atakutana na Rais wa mpito Mitchel Djotodia kiongozi wa zamani wa waasi wa Seleka aliyeingia madarakani baada ya mapinduzi yaliyouangusha utawala wa Francois Bozize mwezi Machi mwaka huu.

Ziara ya kiongozi huyo inakuja siku chache baada ya Rais wa Ufaransa Francois Hollande kufika nchini humo akitokea kuhudhuria kumbukumbu ya kumuenzi Rais wa Kwanza mzalendo wa Taifa la Afrika Kusini Hayati Nelson Mandela.

Akiwa nchini humo Rais Hollande alikiri kuwa oparesheni hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa ili kufikia azma ya kurejesha usalama katika Taifa hilo.

Wanajeshi wawili wa Ufaransa waliuawa mwanzoni mwa juma hili, siku chache baada ya Ufaransa kufikisha idadi ya wanajeshi 1600 waliopelekwa nchini humo kulinda usalama.

Ingawa jeshi la Ufaransa linasema wapiganaji wengi wamesalimisha silaha, bado kuna changamoto kubwa ya kukabiliana na chuki za kidini baina ya Wakristo wengi na waislamu wachache ambao wamechukua uongozi wa nchi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.