Pata taarifa kuu
UFARANSA-ISRAEL-PALESTINA

Hollande: Israel isitishe ujenzi wa makazi katika eneo lenye utata ili kutovuruga mazungumzo ya amani baina yake na Palestina

Rais wa Ufaransa, Francois Hollande ameitaka Israel kukomesha shughuli za ujenzi wa makazi ya Wayahudi katika eneo lenye utata ili kutovuruga mazungumzo ya amani baina yao na Palestina. Katika hotuba yake mjini Ramallah alipokuwa na mwenyeji wake Rais wa mamlaka ya Palestina, Mahmud Abbas, Rais Hollande ameisihi Israel kusitisha ujenzi huo katika ardhi waliyoinyakua baada ya vita ya mwaka 1967.

REUTERS/Majdi Mohammed/Pool
Matangazo ya kibiashara

Tangu kuanza kwa mazungumzo ya moja kwa moja baina ya Israel na Palestina yaliyokuwa yamekwama kwa takribani miaka mitatu, Israel ilitangaza ujenzi wa makazi mapya tangazo ambalo liliibua hisia kali kwa Palestina na Marekani.

Juma lililopita Israel ilitangaza mpango wake wa ujenzi wa makazi mapya 20,000 na baada ya ukosoaji mkubwa Waziri wake Mkuu Benjamin Netanyahu aliagiza kusitishwa kwa mpango huo ili kuepusha mgogoro na jumuiya ya kimataifa.

Licha ya mkanganyiko huo, Rais Abbas amesema mazungumzo ya amani yataendelea katika kipindi cha miezi tisa kama walivyokubaliana na Washington.

Atakaporejea mjini Jerusalem, Hollande anatarajiwa kulihutubia bunge katika hotuba ambayo inatarajiwa kuelezea jinsi Ufaransa itakayojidhatiti kuimarisha usalama nchini Israel.

Serikali ya Ufaransa imesema hotuba ya Hollande pia inatarajiwa kutoa ujumbe mzito juu ya maendeleo ya mchakato wa amani na mpango wa nyuklia wa Iran.

Ziara ya Hollande inakuja siku tatu kabla ya kuanza tena kwa mazungumzo ya mpango wa nyuklia wa Iran mjini Geneva nchini Uswisi, katika awamu iliyopita ya mazungumzo hayo iliyotamatika tarehe 10 Novemba hakukuwa na makubaliano yaliyoafikiwa baina ya pande zote.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.