Pata taarifa kuu
LIBYA

Kerry atetea hatua ya Marekani kufanya Oparesheni nchini Libya

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry ametetea hatua ya Makomandoo wa kijeshi wa taifa lake  kufanya oparesheni nchini Libya na kumkamata gaidi wa Al Qaeda Abu Anas al-Liby jijini Tripoli mwishoni mwa juma lililopita. 

Matangazo ya kibiashara

Kerry anasema kuwa utaratibu wote wa kisheria ulifuatwa na wanajeshi wa Marekani hawakuingia nchini Libya kinyume cha sheria.

Serikali ya Libya inasema inataka Marekani itoe maelezo ya kina kuhusu hatua yake ya kumkamata gaidi wa Al- Qaeda Nazih al-Ragye anayefahamika kwa jina maarufu kama Abu Anas al-Liby jijini Tripoli mwishoni mwa wiki iliyopita bila ya kuwafahamisha.

Waziri Mkuu wa Libya Ali Zeidan, amesema kuwa serikali yake  imeshangazwa na namna oparesheni hiyo ilivyotekelezwa na Makomandoo wa Marekani hata bila ya kushirikishwa kuhusu kukamatwa kwa raia wake.

Marekani inasema Oparesheni hiyo ilituma ujumbe kuwa itaendelea na inaendelea  kupambana na kuwasaka magaidi popote pale walipo duniani.

Abu Anas al-Liby raia wa Libya amekuwa akisakwa na serikali ya Marekani kwa kipindi kirefu kwa kuongoza mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa na Al Qaeda katika Ubalozi wa Marekani jijini Nairobi nchini Kenya na Tanzania mwaka 1998 na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 200.

Aidha, kukamatwa kwa gaidi huyo kumesifiwa pia na Waziri wa Ulinzi wa Marekani Chuck Hagel ambaye amewapongeza Makomandoo hao kwa kuonesha ushapavu wa hali ya juu wakati wa kumkamata gaidi huyo kwa kile anachosema ni jitihada za Marekani kupambana na ugaidi duniani.

Mbali na Libya, nchini Somalia wanajeshi wa Marekani walivamia ngome za Al-Shabab mwishoni mwa wiki iliyopita na kutekeleza mashambulizi kutumia ndege za kivita kuwalenga viongozi wa kundi hilo.

Hata hivyo, jeshi la Marekani liliondoka nchini humo baada ya kushindwa kufanikiwa kuwapata viongozi wa Al-Shabab waliokuwa wanashukiwa kujificha katika mji wa Barawe.

Shambulizi hili linakuja wiki mbili baada ya Al-Shabab kushambulia jengo la kibiashara la Westgate jijini Nairobi nchini Kenya  na kuwauawa zaidi ya watu 70 kwa kuwapiga risasi.

Serikali ya Somalia imetangaza kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Jumuiya ya Kimataifa kulisambaratisha kundi la Al-Shabab.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.