Pata taarifa kuu
KENYA-SOMALIA

Kundi la Wanamgambo la Al Shabab latishia kufanya mashambulizi Kenya iwapo itakaidi amri ya kuondoa Wanajeshi wao Somalia

Kundi la Wanamgambo la Al Shabab lenye maskani yake nchini Somalia limetoa kitisho cha kufanya shambulizi jingine nchini Kenya kutokana na Serikali ya Nairobi kugoma kuondoa wanajeshi wake huko Mogadishu wanaopambana kulitokomeza kundi hilo. Al Shabab kupitia taarifa yao wamesema iwapo Serikali ya kenya itakaidi amri yao ya kuwataka waondoe wanajeshi wao basi wenyewe wataendelea kuandaa na kutekeleza mashambulizi zaidi katika Jiji la Nairobi hadi pale watakaposikilizwa.

Wanamgambo wa Kundi la Al Shabab wakiendelea kufanya doria huku wakijihami kwa silaha
Wanamgambo wa Kundi la Al Shabab wakiendelea kufanya doria huku wakijihami kwa silaha
Matangazo ya kibiashara

Kundi la Wanamgambo la Al Shabab lenye uhusiano na Mtandao wa Al Qaeda ndilo lilitangaza kuhusika na shambulizi la kigaidi kwenye Jumba la Biashara la Westgate ambapo kwa mujibu wa takwimu za Serikali watu 67 waliuawa na wengine 39 hawajulikani walipo.

Taarifa ya Kundi la Wanamgambo la Al Shabab imeeleza uamuzi wa Serikali ya Kenya kukaidi amri ya kuataka kuondoka Mogadishu inaonsha bado hawajapata somo kupitia shambulizi la Westgate.

Al Shabab kupitia taarifa yao wamesema Kenya imeonekana kukaribisha mashambulizi zaidi na umagaji wa damu kutokana na kuendelea kusisitiza wanajeshi wake watasalia nchini Somalia kupambana na Wanamgambo hao.

Onyo hili jipya la Kundi la Wanamgambo la Al Shaba linakuja siku moja baada ya Rais wa Kenya Uhuru Muigai Kenyatta kusisitiza hawatoondoa wanajeshi wao nchini Somalia hadi pale watakapohakikisha kumekuwa na usalama wa kudumu.

Rais Kenyatta amesisitiza hawawezi kuondoa vikasi vyao nchini Somalia kwa sababu waliombwa na Serikali ya Mogadishu kufanya kazi hiyo ya kuimarisha hali ya usalama ambayo haijakamilika bado.

Wanajeshi wa Kenya walianza operesheni yao ya kukabiliana na Kundi la Wanamgambo la Al Shabab baada ya kushuhudia mashambulizi mengi ndani ya nchi yake kabla ya baadaye kujiunga kwenye Kikosi cha Umoja wa Mataifa Kinacholinda Amani AMISOM.

Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi nchini Kenya limekiri kuna miili mingine ya watu iliyopatikana lakini ikiwa imeharibika zaidi na hivyo imeshindwa kutambulika na inahitajika kufanyiwa uchunguzi wa kinasaba.

Miili hiyo imepatikana kutoka ndani ya Jumba la Biashara la Westgate lililokuwa limetekwa kwa siku nne na Wanamgambo wa Al Shabab wanaopata ufadhili kutoka kwa mtandao wa Al Qaeda.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.