Pata taarifa kuu
NIGERIA-BOKO HARAM

Kundi la Boko Haram lawaua Watu 38 katika jimbo la Borno nchini Nigeria

Takribani watu 38 wameuawa na wengine zaidi ya 30 hawajulikani walipo baada ya kushambuliwa na watu wanaodhaniwa kuwa wanamgambo wa Boko Haram katika jimbo la Borno nchini Nigeria mwishoni mwa juma hili. Mwakilishi wa serikali kutoka eneo hilo Alhaji Garba Ali amewaambia waandishi wa habari kuwa watu 14 miongoni mwa waliouawa ni kutoka jamii ya wafugaji.

Reuters
Matangazo ya kibiashara

Kiongozi mmoja ambaye hakutaka jina lake kuwekwa hadharani amesema watu 24 miongoni mwa waliouawa ni wanachama wa vikundi vilivyo katika kampeni ya kupambana na kundi la Boko Haram katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.

Inadaiwa kuwa watu waliokuwa wamevalia sare ya jeshi na kudhaniwa kuwa ni wanajeshi wa serikali ya nchi hiyo walijiunga na kikosi kilichojitolea kupambana na Boko Haram na kuingia nao msituni lakini baadae waliwageuka na kuwashambulia.

Jeshi la nchi hiyo limekuwa likihimiza kuundwa kwa vikundi vitakavyosaidia kuliangamiza kundi hilo lakini jitihada hizo zimekuwa zikididimizwa na mashambulizi yanayowalenga watu hao.

Mwezi Mei mwaka huu Rais Goodluck Jonathan alitangaza hali ya hatari katika majimbo matatu tofauti Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo akisema kuwa kundi la Boko Haram linatishia usalama wa Nigeria.

Mashambulizi yanayoendeshwa na Boko Haram yamesababisha mauaji ya watu zaidi ya elfu tatu na mia sita tangu mwaka 2009, vikosi vya usalama vimekuwa vikilengwa zaidi na wanamgambo hao.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.