Pata taarifa kuu
UMOJA WA MATAIFA-MISRI

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban ataka Mohamed Morsi aachiwe huku maandamano yakitaifa yakitarajiwa kufanyika nchini Misri

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon ametoa wito kwa Serikali ya Misri kumuachia Kiongozi aliyeondolewa madarakani kwa nguvu za Jeshi Mohamed Morsi kipindi hiki nchi hiyo ikijiandaa kufanya maandamano ya kitaifa yaliyoitishwa na Mkuu wa Majeshi Jenerali Abdel Fattah Al Sisi.

Picha ya Kiongozi wa zamani wa Misri Mohamed Morsi ambaye anashikiliwa na Jeshi nchini humo
Picha ya Kiongozi wa zamani wa Misri Mohamed Morsi ambaye anashikiliwa na Jeshi nchini humo REUTERS/Asmaa Waguih
Matangazo ya kibiashara

Ban amesema wakati wa kuachiwa kwa Morsi umefika na iwapo anapaswa kujibu mashtaka yoyote ni bora kitu hicho kifanyike kwa uwazi ili kumaliza hali ya wasiwasi ambao imeendelea kushuhudiwa nchini Misri kutokana na wafuasi wake kupiga kambi mitaani wakifanya maandamano.

Katibu Mkuu wa UN ameweka wazi iwapo Morsi ataendelea kushikiliwa basi itakuwa vigumu kwa nchi hiyo kushuhudia utulivu wa dhati ambao ulikuwepo hapo awali baada ya kuchaguliwa kidemokrasia Kiongozi huyo na kukaa madarakani kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Morsi na Viongozi wengine kadhaa wa Chama Cha Muslim Brotherhood wangali wakishikiliwa na Serikali inayoongozwa na Kiongozi wa Mpito Adly Mahmud Mansour ambaye amepewa jukumu la kuitisha uchaguzi mapema mwakani ili demokrasia ichukue mkondo wake.

Kitendo hicho cha kuendelea kushikiliwa kwa Morsi na Viongozi wengine wa Chama Cha Muslim Brotherhood ndicho kinaonekana chanzo cha uwepo wa maandamano yasiyokishwa kutoka kwa wafuasi wa Chama hicho waliojiapiza kuendelea kupambana hadi pale Kiongozi wao atakaporudishwa madarakani.

Wito wa Ban unakuja kipindi hiki wafuasi wanaopinga Chama Cha Muslim Brotherhood wakijiandaa kufanya maandamano makubwa kuunga mkono serikali mpya na kutoa kibali kwa jeshi kupambana na machafuko yanayoendelea sanjari na vitendo vya kigaidi vinavyoshuhudiwa.

Maandamano hayo ya Kitaifa yaliitishwa na Mkuu wa Majeshi Jenerali Al Sisi ambaye alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi ili kuonesha wanaunga mkono juhudi za jeshi katika kuzima vitendo vyote vy akigaidi vinavyoendelea.

Viongozi kadhaa wa zamani nchini Misri wamekosoa maandamano hayo akiwemo Waziri Mkuu wa zamani Hisham Qandil ambaye ameonya hatua hiyo akisema huenda ikachochea zaidi machafuko katika Taifa hilo.

Naye Kiongozi wa Chama Cha Muslim Brotherhood Mohamed Badie amesema maandamano hayo hayatosaidia kurejesha utulivu na badala yake ametoa wito kwa wananchi kusimama kupigania uhuru na kupinga mapinduzi ya kijeshi yaliyomwaga damu.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.