Pata taarifa kuu
SYRIA-MAREKANI-URUSI

Upinzani wazidi kugawanyika, utawala wa Assad wasema uko tayari kushiriki mazungumzo ya Geneva

Baraza la upinzani nchini Syria limeendelea kuvutana wakati huu ambapo viongozi wake wanaendelea kujadiliana iwapo wahudhurie mkutano wa kimataifa ulioandaliwa na Serikali ya Urusi na Marekani huku utawala wa rais Bashar al-Assad ukitangaza kuwa tayari kushiriki mazungumzo hayo.

Waziri wa mambo ya nje wa Syria, Walid Muallem akiwa na mwenzake wa Iraq, Hoshyar Zebari wakati wa ziara yake nchini Iran na kutangaza nia ya nchi yake kushiriki mazungumzo ya amani
Waziri wa mambo ya nje wa Syria, Walid Muallem akiwa na mwenzake wa Iraq, Hoshyar Zebari wakati wa ziara yake nchini Iran na kutangaza nia ya nchi yake kushiriki mazungumzo ya amani Reuters
Matangazo ya kibiashara

Mazungumzo hayo yanatarajiwa kufanyika juma lijalo mjini Geneva Uswis ambapo pamoja na mambo mengine mkutano huo unatarajiwa kuja na mapendekezo ya namna ya kutatua mzozo wa kisiasa ulioko nchini humo ambapo tayari umegharimu vifo vya watu elfu 90 mpaka sasa.

Katika hatua nyingine kumeshuhudiwa mapigano makali baina ya wapiganaji wa jeshi huru la Syria na wale wanamgambo wa Hezbollah nchini Lebanon ambao wanapigana kwenye mji wa Qusayr wakimuunga mkono rais Bashar al-Assad.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema kuwa usiku wa kuamkia hii leo kumeshuhudiwa mashambulizi ya roketi toka kwa wapiganaji wa Hezbollaha ambapo baadhi ya roketi hizo zimepiga eneo la mpaka wa Lebanon na Israel.

Serikali ya Israel tayari imetangaza kuanzisha uchunguzi kuhusu shambulio la roketi hilo kubaini iwapo limerushwa na wanajeshi wa Serikali au.

Waasi wa Syria wanaonekana kuzidiwa nguvu kwenyemji huo ambao sasa kwa sehemu kubwa umerejeshwa chini ya himaya ya vikosi vya Serikali ya rais Assad ambavyo vilianzisha mashambulizi hivi karibuni dhidi ya ngome zao.

Mashambulizi hayo yanafanyika wakati huu ambapo mawaziri wa mambo ya nje wa Urusi, Marekani na Ufaransa wanakutana hii leo jijini Paris, Ufaransa kujadili namna ya kuondoa mpasuko uliojitokeza ndani ya baraza la upinzani la Syria.

Mkutano wa leo unaenda sambamba na mkutano wa mawaziri wa Umoja wa Ulaya EU, ambao wanakutana kujadili iwapo waondoe vikwazo zaidi vya silaha dhidi ya waasi wa Syria kwa lengo la kuwawezesha kupata silaha zaidi kukabiliana na wanajeshi wa Serikali.

Makataa ya vikwazo vya awali vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya muda wake unamalizika mwishoni mwa mwezi huu.

Wakati upinzani wenyewe ukiendelea na mkutano wao kwa siku ya nne mfululizo kujaribu kuunda Serikali yao ya mpito, hiyo jana waziri wa mambo ya kigeni wa Syria, Walid Muallem ametangaza Serikali yake kuwa tayari kushiriki mazungumzo ya amani na upinzani bila ya masharti toka kwa upinzani.

Utawala wa Syria umeendelea kusisitiza kuwa licha ya mazungumzo hayo, uamuzi wa nani awe kiongozi wa Syria unabakiwa mikononi mwa wananchi wenyewe na sio kufuata matakwa ya upinzani.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.