Pata taarifa kuu
MAREKANI-ISRAELI-PALESTINA

Marekani yajiapiza kusimama kidete kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana Mashariki ya Kati

Serikali ya Marekani imesisitiza itaendelea na juhudi zake za kuhakikisha umwagaji wa damu nchini Syria unakomeshwa huku pia ikifufua mazungumzo ya kusaka amani ya Mashariki ya Kati baina ya Israeli na Palestina.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry akizungumza na Waziri wa Sheria wa Israeli Tzipi Livni
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry akizungumza na Waziri wa Sheria wa Israeli Tzipi Livni
Matangazo ya kibiashara

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry amesema atafanya kila linalowezekana kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana Mashariki ya Kati kitu ambacho kisaidia uwepo wa utulivu katika mataifa mengine ikiwemo nchi ya Syria.

Kerry amesema atarejea tena Mashariki ya Kati katika kipindi cha majuma mawili yajayo kuendelea na harakati zake za kuhakikisha amani inapatikana na majirani Israeli na Palestina wanamaliza ugomvi wao wa miaka mingi.

Kauli ya Kerry ameitoa alipokutana na Mpatanishi wa Israeli Tzipi Livni na kumueleza Marekani imejitolea kuhakikisha amani inapatikana Mashariki ya Kati kupitia njia ya mazungumzo.

Waziri Kerry amejiapiza kusimama kidete kuhakikisha mazungumzo yaliyovunjika mwaka 2010 yanarejeshwa na kuleta manufaa kwa pande hizo mbili ili kumaliza uhasama uliojijenga miongoni mwao.

Kerry amesema atarejea mashariki ya Kati kukutana na Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu na Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmud Abbas lengo ni kuwashawishi kurejea kwenye meza ya mazungumzo.

Mpatanishi wa Israeli Livni amempongeza Waziri Kerry kutokana na kuonesha kuguswa kwake na kukosekana kwa amani ya kudumu katika eneo la Mashariki ya Kati na ameahidi nchi yake itampa ushirikiano wa kutosha.

Livini amesema kinachofanywa hivi sasa na Marekani chini ya Waziri Kerry kitarejea matumaini kwa wananchi wa eneo hilo ambao tayari walishapoteza matumaini ya uwepo wa usalama.

Rais wa Marekani Barack Obama naye ameonekana hayupo nyuma katika kumuunga mkono Waziri Kerry kwani amezungumza na Netanyahu anayezuru China na kumtaka kuhakikisha hali ya usalama inarejea Mashariki ya Kati.

Eneo la Mashariki ya Kati limeendelea kushuhudia machafuko baina ya Isareli na Palestina huku serikali ya Ramallah ikitaka Jerusalem iheshimu mipaka ya mwaka 1967 kitu ambacho ndiyo kitamaliza machafuko hayo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.