Pata taarifa kuu
JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA CONGO-UMOJA WA MATAIFA

Waasi wa M23 Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC wapinga hatua ya Umoja wa Mataifa UN kupeleka Kikosi Maalum Mashariki mwa Taifa hilo

Kundi kubwa la Waasi linalopatikana Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC M23 limejitokeza na kupinga kwa nguvu zake hatua ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UNSC kupitisha azimio la kupeleka Jeshi Maalum katika eneo hilo. Kiongozi wa Kisiasa wa Kundi la M23 Bertrand Bisimwa amesema kuwa kupelekwa kwa kikosi hicho maalum kilichoidhinishwa na wanachama 15 wa kudumu wa Baraza la Usalama hakiwezi kusaidia kurejesha hali ya amani huko Mashariki.

Wanajeshi wa Kundi la Waasi la M23 wakiwa katika Mji wa Goma uliopo Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC
Wanajeshi wa Kundi la Waasi la M23 wakiwa katika Mji wa Goma uliopo Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC REUTERS/James Akena
Matangazo ya kibiashara

Tamko la Kundi la Waasi la M23 limekuja kipindi hiki ambacho Baraza la Usalama limepitisha azimio maalum la kupelekwa kwa Kikosi huko Mashariki mwa DRC kupambana na makundi ya waasi yanayomiliki silaha na kuwa kitisho cha usalama.

Bisimwa amesema Umoja wa Mataifa UN umeamua kuchagua njia ya kivita katika kushughulikia mgogoro wa kisiasa kitu ambacho hakiwezi kikasaidia kurejesha hali ya utulivu huko Mashariki mwa DRC.

Kiongozi huyo wa M23 iliyochini ya Sultan Makenga amesema njia pekee ya kufikia kupatikana kwa amani ya kudumu Mashariki mwa DRC ni kwa kutumia makubaliano badala ya njia za mapigano zilizopendekezwa na Baraza la Usalama.

Kundi la Waasi la M23 limesema matarajio yao yalikuwa ni kwa Baraza la Usalama lingewajumuisha watu ambao wapo tayari kusaka amani ili kuwaweka pamoja na hatimaye kupata utulivu Mashariki mwa DRC lakini imekuwa tofauti.

Waasi wa M23 wameanza kuingiwa na hofu ya kusambaratishwa kutokana na azimio la Baraza la Usalama la kuunda kikosi maalum cha wanajeshi 3,000 kukipa mamlaka ya kupambana na waasi na si kuishia kulinda amani tu kama ilivyo kwa MONUSCO.

Baraza la Usalama limeidhinisha kupelekwa kwa kikosi hicho ambacho kitashirikiana na wanajeshi kutoka Tanzania, Afrika Kusini na Malawi ambao wataenda Mashariki mwa DRC kwa lengo la kulinda amani Mashariki mwa DRC.

Hiki ni kikosi cha kwanza kuidhinishwa na Baraza la Usalama kueleka nchini DRC kukabiliana na makundi ya Waasi na jukumu lao halitakuwa sawa na Majeshi ya Kulinda Amani MONUSCO.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.