Pata taarifa kuu
PAKISTAN

Watu wanne wauawa wakihusishwa na mauaji ya Washia 89 mwishoni mwa juma huku maandamano yakiendelea

Jeshi la Polisi nchini Pakistani limewaua watu wanne na kuwakamata wengine saba ambao wanatuhumiwa kutekeleza mashambulizi yaliyochangia mauaji ya Washia wapatao 89 mwishoni mwa juma. Watu hao wameuawa kwenye operesheni maalum iliyoendeshwa katika Jiji la Quetta ambapo Waziri wa Mambo ya Ndani katika Jimbo la Baluchistan Akbar Hussain Durrani na Kanali Maqbool Ahmed wamethibitisha hilo.

Wanawake wa Jamii ya Washia wakiendelea na maandamano yao wakitaka kumalizwa kwa umwagaji wa damu
Wanawake wa Jamii ya Washia wakiendelea na maandamano yao wakitaka kumalizwa kwa umwagaji wa damu REUTERS/Mohsin Raza
Matangazo ya kibiashara

Viongozi hao wamesema operesheni kabambe ilifanyika katika Mji wa Hazara na hivyo jeshi likafanikiwa kuwaua watuhumiwa hao sambamba na kuwatakama wengine kipindi hiki ambacho maandamano ya Washia yakiendelea.

Maandamano makubwa yameendelea kushuhudiwa nchini Pakistan katika Jiji la Quetta ambapo watu wa jamii ya Kishia wameendelea kuishinikiza serikali kuhakikisha inachukua hatua dhidi ya mauaji ya watu 89 yaliyofanyika mwishoni mwa juma.

Maelfu ya watu wa jamii ya Shia wameendelea kutoa shinikizo hilo sambamba na kukataa kuzika miili ya wenzao ambao wameuawa kwenye mashambulizi ambayo yamekuwa yakitekelezwa kulenga jamii hiyo ndogo.

Zaidi ya wanawake 4,000 wameonekana barabarabi wakifunga njia Kusini Magharibi kwa Jiji la Quetta ikiwa ni sehemu ya kuonesha hasira walizonazo kutoka na kufanyika kwa mauaji hayo mara kwa mara.

Jamii ya watu wa Shia wamejiapiza kuendelea na maandamano yao hadi pale ambapo serikali itasikiliza kilio chao na hatimaye kuwachukulia hatua za kisheria wale waliohusika na mauaji ya mwishoni mwa juma.

Waandamanaji hao wamejitokeza wakiwa na mabango yao yenye ujumbe “Acha Kuwaua Washia” yaliyokuwa yameinuliwa muda wote wa maandamano yao yaliyoambatana na nyimbo za kuhasasisha kuendelea na maandamano hayo.

Jeshi la Polisi nchini Pakistan limesema linaendelea na mkakati madhubuti wa kuhakikisha maandamano hayo yanasitishwa mara moja kwa kuendelea kukutana na Viongozi wa jamii ya Shia.

Chama Cha Waislam cha Washia cha Wahdatul kupitia Makamu wa Rais Amin Shaheedi ametaka uongozi wa Jiji la Quetta uwe chini ya Jeshi ili kuhakikisha hali ya usalama inaimarika na kuzuia mauaji.

Kundi la Wasunni linalotambulika kwa jina la Lashkar-e-Jhangvi ndilo limejitangaza kuhusika na mashambulizi hayo ambayo yaliwaacha watu 178 wakijeruhiwa na kuchangia kuongeza hofu ya kiusalama.

Mashambulizi haya yamekuja ikiwa ni mwezi mmoja tangu kuuwa kwa Washia 95 katika eneo la Hazara kitu ambacho kimewatisha washia wakiamini wamekuwa wakilengwa na mashambulizi yanayofanywa na Wasunni.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.