Pata taarifa kuu
MISRI

Jeshi nchini Misri laonya huenda Taifa hilo likaparaganyika kama ghasia zinazoendelea kushuhudiwa hazitadhibitiwa

Jeshi nchini Misri limeonya mgogoro wa kisiasa ambao unaendelea kushamiri katika Taifa hilo unaweza ukasababisha Nchi hiyo kugawanyika kipindi hiki ambacho idadi ya watu waliopoteza maisha kwenye machafuko hayo ya siku tano ikifika hamsini na wawili. Mkuu wa Majeshi na Waziri wa Ulinzi wa Misri Jenerali Abdel Fattah Al-Sissi amekiri malumbano ya kisiasa na tofauti za kiutawala ambazo zimekuwa zikijitokeza huenda zikawa chanzo cha kuparaganyika kwa Taifa hilo.

Wanajeshi wa Misri wakiendelea kushika doria katika Jiji la Cairo wakiwa tayari kukabiliana na ghasia za aina zozote
Wanajeshi wa Misri wakiendelea kushika doria katika Jiji la Cairo wakiwa tayari kukabiliana na ghasia za aina zozote
Matangazo ya kibiashara

Jenerali Al-Sissi amesema kile ambacho kinaendelea nchini Misri kinatishia kwa kiasi kikubwa mustakabali wa baadaye wa usalama katika nchi hiyo na lazima hatua za haraka zichukuliwe kudhibiti hali hiyo.

Kiongozi huyo wa juu wa Kijeshi nchini Misri ameonya matatizo ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiusalama ambayo yanaikumba nchi hiyo huenda yakawa chanzo cha kutetereka kwa usalama na utulivu wa nchi kwa ujumla.

Onyo la Jenerali Al-Sissi limekuja baada ya duru za kitabibu nchini Misri kutoa takwimu mpya ambazo zinaonesha watu hamsini na wawili wapoteza maisha katika kipindi cha siku tano cha maandamano katika eneo la Port Said, Ismailiya, Suez na Cairo.

Katika machafuko ambayo yametokea jana baina ya waandamanaji na polisi yameshuhudia watu wawili wakipoteza maisha katika Jiji la Port Said huku mtu mmoja kipigwa risasi katika Mji Mkuu Cairo.

Kauli ya Mkuu wa Majeshi Jenerali Al-Sissi imekuja huku tayari Rais Mohamed Morsi akiwa ametangaza siku thelathini za hali ya hatari katika Miji mitatu ya Port Said, Ismailiya na Suez ambapo watu hawatakiwa kutembea usiku.

Hali hiyo ya hatari ambato imetangazwa na Rais Morsi inaonekana kupuuzwa na wananchi kutokana na kuendelea kufanya maandamano ambayo yamekuwa yakigeuka ghasia pindi waandamanaji wanapopambana na polisi.

Utawala wa Rais Morsi ambao umekuja baada ya kuanguka serikali ya Rais Hosni Mubarak umekuwa ukikumbana na ukosoaji wa hali ya juu kutoka kwa wananchi ambao wameonesha kutoridhishwa na mwenendo wake.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.