Pata taarifa kuu
COLOMBIA-UFARANSA

Kundi la FARC la Colombia limemuachia Mwandishi wa Habari wa Ufaransa

Kundi la Waasi lenye siasa za mrengo wa kushoto nchini Colombia la FARC hatimaye limemuachia Mwandishi wa Habari wa Ufaransa ambaye alikamatwa siku thelathini na tatu zilizopita na alikuwa anazuiliwa kwenye msitu unaomilikiwa na Kundi hilo.

Mwandishi wa Habari wa Ufaransa anayefanyia kazi kituo cha France 24 Romeo Langlois aliyekuwa anashikiliwa na Kundi la Waasi la FARC la nchini Colombia
Mwandishi wa Habari wa Ufaransa anayefanyia kazi kituo cha France 24 Romeo Langlois aliyekuwa anashikiliwa na Kundi la Waasi la FARC la nchini Colombia AFP PHOTO/Luis Acosta
Matangazo ya kibiashara

Romeo Langlois ambaye ni Mwandishi wa Habari kutoka Kituo cha Televisheni ya France 24 ameachiwa baada ya kukamatwa akiwa anapiga picha uharibifu wa mahabara ya dawa za kulevya aina ya cocaine iliyofanywa na Jeshi.

Langlois baada ya kuachiwa ameshukuru kwa wale wote ambao wamefanikisha tukio hilo na amesema kila kitu kilikuwa kinakwenda sawa na hana yoyote ambaye anaweza kumlaumu kwenye lile ambalo limemtokea.

Punde baada ya kuachiwa na Waasi wa FARC Langlois akasafirishwa kuelekea Mji Mkuu Bogota kabla ya baadaye kuanza safari ya kueleka nchini Ufaransa ambako ataungana kwa mara nyingine na familia yake.

Langlois amesema wakati yupo chini ya Kundi la Waasi la FARC huko msituni alikuwa anachukuliwa kama mgeni na alikuwa anapata heshima zote kama binadamu na hivyo anashukuru kwa kile ambacho kimetokea kwani hakudhurika.

Kundi la Waasi la FARC limemkabidhi Langlois kwa Timu Maalum ya Shirika la Msalaba Mwekundu Duniani ICRC wakiwa pamoja na Mjumbe wa Ufaransa Jean-Baptiste Chauvin na Mwanaharakati wa Amani wa muda mrefu Piedad Cordoba.

Kuachiwa kwa Langlois kumepokelewa kwa furaha na Rais wa Ufaransa Francois Hollande ambaye hakusita kueleza hisia zake na kutoa shukurani za dhati kwa Mamlaka nchini Colombia, Ubalozi wa Ufaransa uliopo Bogota pamoja na Shirika la Msalaba Mwekundu Duniani ICRC kwa kazi waliyofanya.

Wazazi wa Langlois ambao ni mama yake Aline na baba yake Michel wamezungumza na Kituo Cha Televisheni cha France 24 wakisema muda wote walikuwa na hofu na kuhisi mtoto wao ameuawa au afya yake imekumbwa na matatizo na hivyo baada ya kuachiwa wamepata faraja kubwa.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.