Pata taarifa kuu
SYRIA-MAREKANI-UJERUMANI

Serikali ya Syria yashindwa kuondoa Vikosi vyake mitaani kwa wakati kama walivyokubaliana na Kofi Annan

Umoja wa Mataifa UN imeendelea kuishinikiza serikali ya Syria kutekeleza agizo la kusitisha umwagaji wa damu ambao umedumu kwa kipindi cha miezi kumi na mitatu katika nchi hiyo wakati huu ambapo tarehe ya mwisho ya kuyaondoa majeshi yao kwenye makazi ya watiu ikiwa imefika bila ya hilo kufanyika. Umoja wa Mataifa UN kwa kushirikiana na Mataifa ya Magharibi wameonesha wasiwasi wao ya kwamba serikali ya Damascus haiwezi kutekeleza agizo la kuondoa Majeshi yao kwenye makazi ya watu kama ambavyo waliafikiana na Mpatanishi wa Kimataifa wa Mgogoro wa Syria Kofi Annan.

Vifaru vya Serikali ya Syria vikiwa kwenye mitaa mbalimbali kukabiliana na Wapiganaji wa Upinzani
Vifaru vya Serikali ya Syria vikiwa kwenye mitaa mbalimbali kukabiliana na Wapiganaji wa Upinzani
Matangazo ya kibiashara

Serikali ya Damascus inalaumiwa kwa kupuuza kutekeleza pendekezo la Anna ambalo awali waliridhia kulifanyiakazi kwa wakati lakini hadi muda wa mwisho ambao ulikuwa saa kumi na mbili asubuhi ya leo hakuna kilichofanyika kwa kiwango ambacho kilikuwa kinatarajiwa na Jumuiya ya Kimataifa.

Damascus kwa upande wake imesema kuwa Majeshi yake yamesitisha mashambulizi kuanzia hii leo saa kumi na mbili asubuhi kama ambavyo ilivyopendekezwa na Annan lakini imetoa onyo kali kuwa itarejesha vikosi vyake iwapo wapiganaji wa upinzani watajaribu kutekeleza shambulizi lolote.

Rais wa Marekani Barack Obama na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel katika mazungumzo yao ya simu walikubaliana Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN ambalo lilibariki shughuli za Anna linatakiwa kuchukua hatua zaidi ili kuhakikisha hali ya utulivu iweze kurejea huko Syria.

Taarifa ya Ikulu ya Marekani maarufu kama White House imethibitisha Rais Obama na Kansela Merkel kutoa pendekezo hilo la kuchukuliwa hatua zaidi katika kuhakikisha wanafanikiwa kumaliza umwagaji wa damu ambao umedumu kwa zaidi ya miezi kumi na mitatu sasa.

Katika hatua nyingine wanaharakati wameendelea kuilaumu serikali ya Damascus inayoongozwa na Rais Bashar Al Assad kutokana na kuendelea kufanya mashambulizi asubuhi ya leo ambayo yamechangia watu kujeruhiwa na wengine kupoteza maisha.

Rami Abdel Rahman ambaye ni Kiongozi kutoka Shirika la Kutetea Haki za Binadamu yenye maskani yake nchini Uingereza amesema watu ishirini na watano wamepoteza maisha kwenye mashambulizi hayo wakiwemo wapiganaji kumi kutoka kwa Wapinzani.

Takwimu za Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa UN zinaonesha kuwa watu zaidi ya elfu tisa wamepoteza maisha tangu kuzuka kwa machafuko nchini Syria kipindi cha miezi kumi na mitatu iliyopita.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.