Pata taarifa kuu
SYRIA

Maandamano makubwa yafanyika nchini Syria baada ya serikali ya Rais Assad kusitisha mashambulizi kutekeleza mapendekezo ya Annan

Maelfu ya wananchi nchini Syria wameandamana kuitikia wito wa Upinzani ambao uliwataka kufanya hivyo kwa lengo la kupima kama kweli serikali ya Rais Bashar Al Assad imetekeleza kwa vitendo hatua ya kusitisha mashambulizi yao licha ya kuendelea kuacha vikosi vyao kwenye makazi ya watu. Msemaji wa Jeshi la upinzani Kanali Kassem Saadeddine amesema wao wamesitisha mapambano licha ya taarifa kusema bomu lililotegwa barabarani kuasababisha kifo cha mwanajeshi mmoja na kujeruhi wengine ishirini na wanne wakiwa kwenye doria shambulizi ambalo limetajwa kuwa ni la kigaidi na serikali.

Wanajeshi wa Syria wakiendelea kuwepo kwenye mitaa mbalimbali licha ya serikali yao kusitisha mashambulizi dhidi ya Wapinzani
Wanajeshi wa Syria wakiendelea kuwepo kwenye mitaa mbalimbali licha ya serikali yao kusitisha mashambulizi dhidi ya Wapinzani
Matangazo ya kibiashara

Taarifa kutoka nchini Syria zimethibitisha kuwa serikali nchini humo imesitisha mashambulizi yake ambayo yamedumu kwa miezi kumi na mitatu lakini imekataa kuondoa vikosi vyao kwa kuhofia huenda Wapinzani wakaanzisha mashambulizi ili waweze kujibu kwa wakati.

Naye Msemaji wa Baraza la Taifa la Syria Bassma Kodmani amesema ni kweli serikali ya rais Assad imesitisha mashambulizi lake lakini hawana hakika kama wamefanya hivyo moja kwa moja kutokana na kuendelea kuona silaha nzito kwenye baadhi ya miji yenye watu wengi.

Haya yanakuja wakati Umoja wa Mataifa UN ukiendelea kuishinikiza serikali ya Syria kutekeleza agizo la kusitisha umwagaji wa damu ambao umedumu kwa kipindi cha miezi kumi na mitatu katika nchi hiyo wakati huu ambapo tarehe ya mwisho ya kuyaondoa majeshi yao kwenye makazi ya watiu ikiwa imefika bila ya hilo kufanyika.

Umoja wa Mataifa UN kwa kushirikiana na Mataifa ya Magharibi wameonesha wasiwasi wao ya kwamba serikali ya Damascus haiwezi kutekeleza agizo la kuondoa Majeshi yao kwenye makazi ya watu kama ambavyo waliafikiana na Mpatanishi wa Kimataifa wa Mgogoro wa Syria Kofi Annan.

Serikali ya Damascus inalaumiwa kwa kupuuza kutekeleza pendekezo la Anna ambalo awali waliridhia kulifanyiakazi kwa wakati lakini hadi muda wa mwisho ambao ulikuwa saa kumi na mbili asubuhi ya leo hakuna kilichofanyika kwa kiwango ambacho kilikuwa kinatarajiwa na Jumuiya ya Kimataifa.

Damascus kwa upande wake imesema kuwa Majeshi yake yamesitisha mashambulizi kuanzia hii leo saa kumi na mbili asubuhi kama ambavyo ilivyopendekezwa na Annan lakini imetoa onyo kali kuwa itarejesha vikosi vyake iwapo wapiganaji wa upinzani watajaribu kutekeleza shambulizi lolopte.

Rais wa Marekani Barack Obama na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel katika mazungumzo yao ya simu walikubaliana Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN ambalo lilibariki shughuli za Anna linatakiwa kuchukua hatua zaidi ili kuhakikisha hali ya utulivu iweze kurejea huko Syria.

Taarifa ya Ikulu ya Marekani maarufu kama White House imethibitisha Rais Obama na Kansela Merkel kutoa pendekezo hilo la kuchukuliwa hatua zaidi katika kuhakikisha wanafanikiwa kumaliza umwagaji wa damu ambao umedumu kwa zaidi ya miezi kumi na mitatu sasa.

Katika hatua nyingine wanaharakati wameendelea kuilaumu serikali ya Damascus inayoongozwa na Rais Bashar Al Assad kutokana na kuendelea kufanya mashambulizi asubuhi ya leo ambayo yamechangia watu kujeruhiwa na wengine kupoteza maisha.

Rami Abdel Rahman ambaye ni Kiongozi kutoka Shirika la Kutetea Haki za Binadamu yenye maskani yake nchini Uingereza amesema watu ishirini na watano wamepoteza maisha kwenye mashambulizi hayo wakiwemo wapiganaji kumi kutoka kwa Wapinzani.

Takwimu za Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa UN zinaonesha kuwa watu zaidi ya elfu tisa wamepoteza maisha tangu kuzuka kwa machafuko nchini Syria kipindi cha miezi kumi na mitatu iliyopita.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.