Pata taarifa kuu
SYRIA-USWISS

Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa UN yataka kusitishwa kwa mapigano Nchini Syria

Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa UN imetaka mapigano ambayo yanaendelea kushuhudiwa nchini Syria na kugharimu maisha ya watu wasio na hatia yasitishwe mara moja wakati huu ambapo Azimio la kudhibiti mauaji likiendelea kuandaliwa.

Mkuu wa Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa UN Navi Pillay akitoa ripoti ya hali ilivyo nchini Syria
Mkuu wa Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa UN Navi Pillay akitoa ripoti ya hali ilivyo nchini Syria REUTERS/Denis Balibouse
Matangazo ya kibiashara

Mkuu wa Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa UN Navi Pillay amesema kuwa kinachofanyika kwa sasa nchini Syria ni cha kulaaniwa kwa nguvu zote kwani wananchi wanaendelea kuteseka kutokana na mashambulizi yanayofanyika huko Homs.

Pillay ameuambia mkutano wa Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa UN huko Geneva nchini Uswiss kuwa hali imekuwa mbaya kwani wananchi wanakosa huduma muhimu ikiwemo matibabu, chakula na maji kitu ambacho kinaweza kuchangia vifo zaidi.

Wakati mkutano huo ukilaani kile ambacho kinaendelea nchini Syria nayo nchi ya Ufaransa kupitia kwa Waziri wake wa Mambo ya Nje Alain Juppe ameziangukia China na Urusi kukubaliana na kupitishwa kwa azimio jipya la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN kudhibiti mauaji.

Juppe amesema nchi hizo ambazo zimekluwa zikitumia kura yake ya turufu ya veto kupinga maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja Mataifa UN wanatakiwa kujua namna ambavyo wananchi wanavyoteseka kutokana na hali ya kibinadamu kuzidi kuwa mbaya.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa Bernard Valero amesema wanamatumaini Urusi na China wakati huu watakuwa upande wao na kuweza kuridhia azimio hilo ili kusitisha mauaji na huduma za misaada ziweze kuwafikia wananchi kwa wakati.

Waziri Juppe amesema anahisi Urusi inaweza ikalegeza msimamo wake wakati huu kutokana na nchi hiyo kuwa kwenye harakati za kufanyika kwa uchaguzi wa rais kitu ambacho kinaweza kikawafanya wabadili msimamo wao.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa UN Pillay watu wanaofikia elfu saba na mia sita wamepoteza maisha nchini Syria tangua kuanza kwa maandamano ya kuupinga Utawala wa Rais Bashar Al Assad miezi kumi na moja iliyopita.

Β 

Β 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.