Pata taarifa kuu
SYRIA

Zoezi la kuhesabu kura za maoni kubadili Katiba nchini Syria laendelea

Zoezi la kuhesabu kura za maoni zilizopigwa na Wananchi wa Syria kwa ajili ya kuruhusu mabadiliko ya Katiba linaendelea na matokeo yake yanatarajiwa kutangazwa baadaye hii leo licha ya Upinzani na Mataifa ya Magharibi yakikashifu vikali zoezi hilo.

Zoezi la kuhesabu kura likiendelea nchini Syria baada ya kupigwa kura ya maoni na matokeo yanatarajiwa kutangazwa jumatatu
Zoezi la kuhesabu kura likiendelea nchini Syria baada ya kupigwa kura ya maoni na matokeo yanatarajiwa kutangazwa jumatatu
Matangazo ya kibiashara

Watu zaidi ya milioni kumi na nne wenye umri wa zaidi ya miaka kumi na nane wameshiriki kwenye zoezi la upigaji kura hiyo ya maoni ya kubadili Katiba ambapo kulikuwa na jumla ya vituo elfu kumi na tatu na mia nane na thelathini na tano.

Kabla ya kura hiyo ya maoni haijapigwa hapo jumapili kulikuwa na kampeni nzito ya kuwashawishi wananchi wa taifa hilo kutoshiriki kwenye zoezi la upigaji kura ili kulikwamisha likiongozwa na Viongozi wa Upinzani pamoja na Wanajeshi walioasi.

Serikali ya Rais Bashar Al Assad imeamua kuitisha kura hiyo ya maoni ili kuruhusu mchakato wa mabadiliko kuchukua nafasi kama ambavyo imekuwa ikishinikizwa na wananchi wa taifa hilo kwa zaidi ya miezi kumi na moja sasa.

Dhumuni la kufanyika kwa kura hiyo ya maoni ni kutaka kuandika historia mpya nchini Syria na kuruhusu kufanyika kwa uchaguzi ambao utazishirikisha vyama vingi nchini humo wakati huu ambapo umwagaji wa damu ukiendelea katika Jiji la Homs na Daraa.

Kabla ya kufanyika kwa kura hiyo ya maoni Rais Assad aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili kutumia nafasi yao kidemokrasia kuamua iwapo wafanye mabadiliko ya katiba na kuruhusu uchaguzi ufanyike baadaye mwaka huu.

Mataifa ya Magharibi yakijumisha Marekani, Canada na Ujerumani wamekashifu vikali zoezi hilo la upigaji kura wakisema halina umuhimu kutokana na serikali ya Rais Assad kuendelea kuua raia wasio na hatia.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton akimaliza ziara yake Barani Afrika amelaani vikali Utawala wa Rais Assad pamoja na wanajeshi wanaomuunga mkono akisema wanashiriki kwenye mauaji ya raia wasio na hatia.

Katika hatua nyingine Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu limesema halijafanikiwa kuingia kwenye Jiji la Homs kutoa huduma na misaada kwa wanachi ambao wanaathirika na mashambulizi ya mabomu yanayoendelea.

Shirika la Msalaba Mwekundu limekiri kuendelea kukabiliana na vikwazo vya kufika katika Jiji la Homs kuwafikia wanahabari ambao wamejeruhiwa pamoja na miili ya wengine wawili waliopoteza maisha.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.