Pata taarifa kuu
SYRIA-DAMASCUS

Watu 40 wauawa katika shambulio la bomu mjini Damascus, Syria

Watu zaidi ya Arobaini wameripotiwa kuuawa nchini Syria kufuatia mashambulizi mawili tofauti ya mabomu katika mji mkuu wa Damascus.

Baadhi ya wananchi wakisaidia kuwaokoa watu walioumia kwenye shambulio la bomu mjini Damascus
Baadhi ya wananchi wakisaidia kuwaokoa watu walioumia kwenye shambulio la bomu mjini Damascus Reuters
Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha taifa nchini Syria, kimesema kuwa mabomu mawili yalilipuliwa mjini Damascus katika majengo ya ofisi za usalama wa taifa na makao makuu ya polisi na kusababisha vifo hivyo.

Polisi wamesema kuwa askari na wanajeshi ni miongoni mwa watu ambao wamefariki dunia katika shambulio hilo ambalo watekelezaji wake walitumia magari mawili tofauti.

Ripoti za awali toka nchini humo zinasema kuwa huenda watu waliohusika kwenye shambulio hilo wakawa ni wafuasi wa kundi la kigaidi duniani la Al-Qaeda linalotumia mwanya huu wa machafuko kutekeleza azama yao.

Shambulio hilo linatekelezwa wakati ambapo tayari waangalizi toka Umoja wa nchi za Kiarabu wameanza kuwasili nchini humo ambapo kundi la watu saba liliwasili hapo jana na wengine kati ya 40 na 50 wanatarajiwa kuwasili nchini humi jumamosi hii.

Wakati waangalizi hao wakiwasili, wanaharakati nchini humo wameitisha maandamano ya nchi nzima kupinga hatua ya waangalizi hao kuingia nchini humo wakitaka kwanza utawala wa rais Bashar al-Asad uondoke madarakani.

Hapo jana msemaji wa wanaharakati hao walioko nchini Uturuki alinukuliwa akisema kuwa wanapinga ujumbe wa waangalizi hao toka Umoja wa Kiarabu wakiamini kwamba unalengo la kuendelea kuiunga mkono serikali iliyoko madarakani.

Katika kuonekana kuitikia wito wa wanaharakati maelfu ya wananchi wameanza maandamano katika miji ya Hama, Homs na miji mingine kushinikiza kuondoka nchini humo kwa waangalizi hao kutoka Umoja wa nchi za Kiarabu.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.