Pata taarifa kuu
UINGEREZA-UJERUMANI-UFARANSA

Waziri Mkuu wa Uingereza kuhojiwa na Bunge baada ya kukataa kusaini Mkataba wa Umoja wa Ulaya EU

Bunge Nchini Uingereza linatarajiwa kumpa wakati mgumu Waziri Mkuu David Cameron wakimtaka aeleze ni kwa nini alikataa kutia saini Mkataba wa Umoja wea Ulaya EU kuhusu kuongeza madaraka kwa nchi zenye nguvu kiuchumi pamoja na njia madhubuti za kukabiliana na madeni kwa nchi wanachama.

Matangazo ya kibiashara

Waziri Mkuu Cameron alikataa kusaini mkataba huo pale ambapo nchi wanachama ishirini na saba zinazounda Umoja wa Ulaya EU zilipokutana mwishoni mwa juma lililopita huko Brussels nchini Ubelgiji kwa madai ya kwamba matakwa ya nchi yake hayajazingatiwa.

Kiongozi huyo wa serikali ya Uingereza aliwaambia wanachama ishirini na saba kuwa taifa lao halipo tayari kuweka hatarini uchumi wao kutokana na kusaini mkataba huo mpya ambao hautakuwa na manufaa yoyote kwa nchi hiyo kiuchumi na hata kwa soko lake.

Licha ya Ujerumani na Ufaransa kutumia muda mrefu kupigia chapuoo kupitishwa kwa mkataba huo lakini Waziri Mkuu Cameron akaendelea kuupinga na kusimama imara kutaka maslahi ya nchi yake yazingatiwe kabla ya kusaini mkataba huo kwa maslahi ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya EU.

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel walionekana kuchukizwa na hatua ya Waziri Mkuu Cameron kupinga mpango wao wa kutaka kupitishwa kwa mkataba huo ambao ungeleta suluhu ya mgogoro na hata hatima ya sarafu ya euro.

Wabunge wa Uingereza nao wakakosoa vikali msimamo ambao ulioneshwa na Waziri Mkuu wao wa kupinga kusaini mkataba huo na ndiyo wameamua kutaka kupatiwa maelezo ya kutosha ili wajue sababu za kukataliwa kwa mkataba huo muhimu kwa mataifa wanachama wa EU.

Naibu Waziri Mkuu wa Uingereza Nick Clegg ni miongoni mwa wale ambao wamekosoa uamuzi huo wa Cameron huku akisema kuwa nchi yao huenda ikatengwa na mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya EU na itakuwa hatari.

Kiongozi wa Upinzani Ed Miliband ni miongoni mwa wale ambao wamepingana na uamuzi wa Caneron huku akimtuhumu kutoitakia mema Uingereza kutokana na kuwa nchi pekee ambayo imepinga kusaini mkataba huo licha ya wanachama wengine kurudhia.

Mataifa wanachama ishirini na saba ya Umoja wa Ulaya EU pamoja na wale kumi na saba ambao wanatumia sarafu ya euro walikuwa katika mkutano wa kujadili hatima ya madeni kwenye Ukanda huo sambamba na hatima ya sarafu ya euro.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.