Pata taarifa kuu
UTURUKI

Waokoaji nchini Uturuki wafanikiwa kuwapata watu watatu wakiwa hai akiwemo mtoto mdogo

Kikosi cha Uokoaji nchini Uturuki kimefanikiwa kuhitimisha siku ya jumanne kwa kuwaokoa watu watatu akiwemo mtoto mmoja mwenye siku kumi na nne, mama wa mtoto huyo pamoja na bibi yake ambao wamaelezwa kukwama kwa siku mbili kwenye vifusi tangu nchi hiyo ipigwe na tetemeko la ardhi siku ya jumapili.

REUTERS/Stringer/Turkey
Matangazo ya kibiashara

Watu hao watatu wameokolewa katika Mji wa Ercis na kulikuwa na tofauti ya saa mbili kwa wafanyakazi hao wa kikosi cha uokoaji kuweza kuwaokoa watu hao kutoka katika masalia hayo ya vifusi.

Twakimu ambazo zimetolewa na serikali ya Uturuki zinaonesha kuwa watu mia tatu na sabini wameshapoteza maisha wakati wengine elfu moja na mia tatu wakijeruhiwa katika maeneo ya Ercis na Van ambayo yamepigwa na tetemeko la ardhi lenye kipimo cha saba nukta mbili.

Mtoto huyo mwenye umri wa siku kumi na nne ambaye ametambulika kwa jina la Azra Karaduman aliokolewa na kisha kuwahishwa hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu kabla ya baadaye kuokolewa mama yake mzazi anayeitwa Seniha.

Zoezi la ukoaji lilipoendelea ndiyo waokoaji wakafanikiwa kumuokoa bibi wa mtoto huyo mwenye umri wa miaka sabini na mitatu ambaye ametambulika kwa jina la Gulzade Karaduman ambaye naye anapatiwa matibabu katika Hospital ya Ankara.

Kuokolewa kwa watu hao wakiwa hai kurejesha matumaini ya kikosi cha waokoaji kuweza kuwapata watu zaidi waliohai baada ya hapo awali kuamini hakuna mtu mwingine ambaye atakuwa mzima baada ya kupita siku mbili za msako.

Kwa upande wake Naibu Waziri Mkuu wa Uturuki Besir Atalay amethibitisha idadi ya vifo kuongezeka na kufikia watu mia tatu na sabini kutoka mia tatu na sitini na sita iliyokuwa hapo awali.

Tayari misaada imeanza kusambazwa kwa waathirika wa tetemeko hilo la ardhi ambalo lilitokea siku ya jumapili ambapo mahema yameanza kufikishwa katika majiji ya Ercis na Van pamoja na vijiji vya jirani.

Umoja wa Mataifa UN kupitia kwa Katibu Mkuu wake Ban Ki Moon umeeleza kusikitishwa kwake na tetemeko hilo na imesema itakuwa tayari kutoa msaada iwapo utahitajika na serikali ya Uturuki.

Waziri Mkuu Reccep Tayyip Erdogan alizuru eneo lililokumbwa na tetemeko la ardhi na kuwaahidi wananchi ya kwamba serikali kitakuwa bega kwa bega na wananchi ambao wamekumbwa na madhara ya tukio hilo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.