Pata taarifa kuu
KENYA-UHOLANZI

Mawaziri wa zamani wa Kenya na Mwandishi wa Habari kupanda kizimbani Hague kujua hatima yao kama wana kesi ya kujibu

Mawaziri wawili wa zamani wa Kenya pamoja na Mwandishi wa Habari mmoja wanakuwa watuhumiwa wa kwanza watatu wanaotuhumiwa kuhusika kwenye kupanga ghasia za baada ya uchaguzi nchini mwao kufikishwa Mahakama ya Uhalifu wa Kivita ICC kujua hatma yao iwapo wanakesi ya kujibu au la.

Matangazo ya kibiashara

Mawaziri hao wa zamani ni pamoja na Waziri wa Elimu ya Juu William Ruto, Henry Kosgey ambaye alikuwa Waziri wa Viwanda na Mwandishi Joshua Arap Sang ambao watakuwa kwenye wakati mgumu kufahamu majaaliwa ya kesi yao.

Watuhumiwa hao watatu wa kupanga na kuchochea machafuko ya baada ya uchaguzi wa Rais mwaka elfu mbili na saba wataingia Mahakamani mapema asubuhi ya leo ambapo Waendesha Mashtaka watakuwa na kibarua kigumu cha kuweka bayana vithibitisho.

Ruto, Kosgey na Sang wote walikuwa ni wafuasi wa Mgombea wa Upinzani kwenye kinyang'anyiro hicho ambaye kwa sasa ni Waziri Mkuu Raila Amolo Odinga ambaye alikuwa anakabiliana na Rais Mwai Emilio Kibaki.

Mahakama ya ICC itakuwa na wakati wa kutosha kusikiliza kwa kina ushahidi wa namna ambavyo watuhumiwa hao watatu wa kwanza walivyohusika kwenye kuchochea ghasia hizo kwani watakamilisha zoezi hilo tarehe 12 ya mwezi Septemba.

Tayari wanasheria upande wa utetezi wameshawasilisha orodha ya majina arobaini na nae ya mashahidi ambao wanaweza kutoa uthibitisho wa kile ambacho kilitokea wakati wa ghasia hizo zilizosababisha vifo vya watu zaidi ya elfu moja.

Ikikamilika ungwe ya kwanza ya kusikiliza ushahidi wa watuhumiwa hao watatu ICC itaanza kusikiliza ushahidi mwingine wa watuhumiwa waliosalia ambao utaanza rasmi tarehe 21 ya mwezi Septemba.

Kwenye kundi hilo wanatarajiwa kuwepo Waziri wa Fedha Uhuru Kenyatta, Mkuu wa zamani wa Jeshi la Polisi Mohammed Hussein Ali pamoja na Mkuu wa Huduma za Umma Francis Muthaura.

00:10

Waziri wa zamani wa Elimu ya Juu William Ruto akikanusha kuhusika na machafuko

Wakati Ruto akiondoka nchini Kenya ameendelea kukanusha kuhusika kwa namna yoyote kuchochea na kupanga machafuko yaliyoibuka baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 na saba.

Ruto ambaye anatajwa kusaka urais kwenye uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2012 amekuwa akikana na kudai hakuna ushahidi wowote unaomtia hatiani yeye kutekeleza tuhuma ambazo anasingiziwa kuzifanya.

Naye Mwandishi wa Habari pekee kwenye kesi hiyo Sang anakana kuwepo hata kwenye eneo la tukio siku ya machafuko na badala yake alikuwa ofisi akiendelea na kazi zake sasa anashangazwa na hatua hiyo.

Ghasia hizo zilizokuwa kwenye mrengo wa kikabila zilisababisha zaidi ya watu elfu moja na mia mbili wapoteze maisha huku wengine zaidi ya laki tatu wakilazimika kuyahama makazi yao kukimbia mapigano hayo.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.