Pata taarifa kuu
YEMEN

Rais wa Yemen Ali Abdullah Saleh aapa kulipiza kisasi kwa watu waliomshambulia na kumjeruhi

Kwa mara ya kwanza rais wa Yemen Ali Abdullah Saleh amelihutubia taifa kupitia njia ya televisheni na kuapa kulipiza kisasi kwa watu walioshambulia makazi yake na kumjeruhi siku ya ijumaa.

Rais wa Yemen Ali Abdallah Saleh akihutubia taifa mapema leo asubuhi
Rais wa Yemen Ali Abdallah Saleh akihutubia taifa mapema leo asubuhi Reuters/Yémen TV
Matangazo ya kibiashara

Hotuba hiyo ambayo ilirushwa usiku wa kuamkia leo, rais Saleh amewashutumu vikali viongozi wa makabila akisema kuwa kwa kiasi kikubwa wao ndio wamechangia kuendelea kwa machafuko nchini humo.

Kiongozi huyo ambaye alikimbizwa katika hospitali  moja ya kijeshi katika mji wa Sanaa kwa matibabu amesema kuwa shambulio hilo liliwaua maofisa wake sita wa usalama ambao walikuwa wakilinda eneo la msikiti ambao alikuwa akitumia kusali.

Shambulio hilo lilifanywa na watu wasiojulikana katika makazi ya rais ulipo msikiti ambao rais Saleh amekuwa akiutumia kusali yeye pamoja na maofisa wengine ambapo alipata majeraha kadhaa mwilini huku maofisa wake sita wakipoteza maisha.

Rais Saleh katika hotuba yake amesifu vikosi vyake akisema kuwa tangu kuanza kwa machafuko nchini humo vikosi vyake vimekuwa vikiwajibika kikamilifu katika kukabiliana na wapiganaji wa kikabila ambao wanaendelea na mashambulizi dhidi ya majeshi yake kwa lengo la kutaka kumg'oa madarakani.

Kiongozi huyo ameongeza kuwa atahakikisha kuwa wote waliohusika katika shambulio hilo wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria, huku pia safari hii akiviagiza vikosi vyake kutumia nguvu zaidi katika kukabiliana na wafuasi ambao wanafanya maandamano kumpinga huku wakitumia silaha.

Polisi nchini humo wamesema kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa watu waliohusika na shambulio hilo ni wale wanajeshi watiifu wa Sheikh Sadiq al-Ahmar kiongozi wa juu kabisa wa upinzani nchini humo.

Shambulio hilo limekuja ikiwa zimepita saa chache tangu vikosi vya serikali vishambulie makazi ya kiongozi huyo ambapo wachambuzi wa mambo wanasema kuwa shambulio hili huenda likawa ni lakulipiza kisasi kwa kile ambacho wanajeshi wa serikali walikifanya.

Wakati huohuo serikali ya Ujerumani imetangaza kufunga ubalozi wake nchini humo na kumuagiza balozi wake kurejea nyumbani kwa kile ilichoeleza ni hali mbaya ya usalama inayoendelea nchini humo.

Jumuiya ya kimataifa mara kwa mara imekuwa ikilaani vurugu zinazoendelea nchini humo wakimtaka Rais Saleh kukubali kung'atuka madarakani kwa mkataba maalumu ambao hata hivyo kiongozi huyo amekuwa akishindwa kutia saini makubaliano ya maazimia ya nchi za Ghuba ambazo zlimtaka kubakia madarakani kwa mwezi mmoja kupisha serikali ya mseto ikiwa ni pamoja na yeye kutochukuliwa hatua za kisheria pindi akiachia madaraka.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.