Pata taarifa kuu
PAKISTANI

Pakistani yakana kupokea ombi la Serikali ya Marekani kutaka kukutana na ndugu wa Osama Bin Laden

Serikali ya Pakistani imesema haijapokea ombi rasmi kutoka kwa serikali ya Marekani ili kuwapa idhini ya kukutana na ndugu wa aliyekuwa Kiongozi wa Mtandao wa Al Qaeda Osama Bin Laden.

Waziri Mkuu wa Pakistani Yousuf Raza Gilani akiwahutubia wabunge wa nchi hiyo
Waziri Mkuu wa Pakistani Yousuf Raza Gilani akiwahutubia wabunge wa nchi hiyo REUTERS/Prime Minister's Office/Handout
Matangazo ya kibiashara

Wizara wa Mambo ya Nje wa Pakistani kupitia Msemaji wake Tehmina Janjua imesema haijapokea taarifa yoyote kutoka serikali ya Marekani inayoomba kukutana na ndugu wa Marehemu Osama Bin Laden.

Janjua hakuishia hapo bali amesema hata nchi nyingine ambazo ndiyo asili ya ndugu wa Osama Bin Laden ambazo ni Yemen na Saudi Arabia nazo hazijatuma maombi yoyote ya kutaka kukutana na jamaa hao.

Kauli hii inakuja baada ya hapo awali kuwa na fununu ya kwamba Pakistani ingeiruhusu Marekani kukutana na wake watatu wa Osama Bin Laden ili iweze kuwahoji juu ya kile ambacho wanakifahamu juu ya Mtandao wa Al Qaeda.

Marekani imekuwa na hamu ya kukutana na wake hao wa Osama kwa kile ambacho kinaelezwa watakuwa na siri kubwa juu ya mipango ambayo alikuwa nayo mume wao katika kutekeleza mashambulizi mbalimbali duniani.

Mmoja wa wake wa Osama ambaye naye alipigwa risasi ya mguu wakati wa operesheni ya kufanikisha kifo cha mume wake aliwaambia Wachunguzi wa Pakistani kwamba waliishi kwa kipindi cha miaka mitano karibu na kambi ya kijeshi.

Tayari Msemaji wa Ikulu ya Marekani Jay Carney amenukuliwa akisema anatamani wapate nafasi ya kuwahoji wake hao wa Osama Bin Laden kwa kuwa anaamini wanasiri kubwa na hata kujua baadhi ya nyaraka muhimu.

00:46

Jay Carney Akizungumzia uhusiano wa Marekani na Pakistani baada ya Kifo cha Osama Bin Laden

Carney aliweka wazi kuwa ni wazi kwa sasa uhusiano baina ya Marekani na Pakistani umetetereka lakini watajitahidi kuuimarisha kwa kuwa una umuhimu mkubwa sana.
Mapema siku ya jumatatu Waziri Mkuu wa Pakistani Yousuf Raza Gilani aliliambia Bunge la nchi hiyo taifa lake halitakiwi kulaumiwa kutokana na Osama Bin Laden kuuawa katika taifa lake bali lawama hiyo inastahili kubebwa na duniani nzima.

Tangu kutokea kwa kifo cha Kiongozi wa Mtandao wa Al Qaeda Osama Bin Laden kilichofanikishwa na Makomandoo wa Marekani kumekuwa na masuala mengi tata yaliyojitokeza kubwa likiwa ni kutetereka kwa uhusiano wa Pakistani na Marekani.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.