Bangladesh: Siku ya tatu ya makabiliano makali ya kidini kati ya Wahindu na Waislamu
Kwa siku ya tatu mfululizo, Bangladesh inakumbwa na mivutano ya kidini kati ya Waislam walio wengi na Wahindu walio wachache, makabiliano ambayo yamesababisha vifo vya watu 4 na wengine 150 wamejeruhiwa.
Imechapishwa:
Baada ya vitendo vya uharibifu wa maeneo ya ibada ambavyo vilibadilika kuwa mapigano huko Dhaka na Chittagong, hasa, maelfu ya waumini wameandamana Ijumaa (Oktoba 15) katika mji mkuu dhidi ya kile wanachokiona kama tusi kwa Uislamu.
Chanzo cha vurugu hiyo ni video ambayo imesamba kwenye mitandao ya kijamii. Inaonyesha nakala za kitabu kitukufu kwa Waislamu, Quran, zikiwekwa chini ya mguu wa mungu wa Wahindu.
Siku ya Jumatano Oktoba 13, wakati Wahindu walisherehekea Durga Puja, sikukuu yao kubwa ya kidini huko Bangladesh, umati wa watu wasiopungua 500 walivamia kanisa ya Wahindu huko Hajiganj. Kutokana na tukio hilo, polisi waliwafyatulia risasi umati wa watu, na kusababisha vifo vya watu wanne.
Huo ndio ulikuwa mwanzo wa mapigano makali ya kidini yaliyoambatana na mfululizo wa uharibifu na vitendo vya uharibifu dhidi ya maeneo ya ibada ya Wahindu. Kwa jumla, mahekalu 80 yalishambuliwa au kuteketezwa kwa siku tatu.