Kiongozi wa Myanmar aonya majaji wa ICJ kutoruhusu kuendelea kwa kesi dhidi ya nchi yake
Kiongozi wa Myanmar Aung San Suu Kyi amewataka majaji kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki kutupilia mbali kesi ya mauaji ya kimbari dhidi ya nchi yake.
Imechapishwa:
Kiongozi huyo ameonya kuwa kuendelea kwa kesi hiyo kutachochea mzozo zaidi ambao mpaka sasa umesababisha karibu robo milioni ya waislamu jamii ya Rohingya kukimbia nchi hiyo.
Akihitimisha utetezi wake mbele ya mahakama hiyo, Aung San Suu Kyi alitoa onyo kali kwa majaji ikiwa wataruhusu kuendelea kwa kesi iliyowasilishwa na nchi ya Gambia dhidi ya Myanmar, akisema itadumaza mchakato wa maridhiano.
Suu Kyi ambaye wakati mmoja alikuwa muhanga wa vitendo vya unyanyasaji wa wanajeshi wa nchi hiyo na kumfanya ashinde tuzo ya amani ya Nobel, ndio amekuwa mstari wa mbele safari hii kuwatetea kwa makosa waliyotekeleza dhidi ya jamii ya Rohingya nchini Mwake.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu na hata wajumbe wa kamati ya tuzo ya amani ya Nobel, sasa wanataka tuzo aliyopewa kiongozi huyo ifutwe na achukuliwe kama mmoja wa watu wanaoshiriki kuwaficha wahalifu wa vitendo vya ukatili dhidi ya binadamu.