Pata taarifa kuu
PAKISTAN-MAREKANI

Pakistan yaionya Marekani kutorudia uvamizi wa kijeshi bila usalama wa taifa kufahamu

Wabunge nchini Pakistan wameionya nchi ya Marekani kutorudia tena kitendo cha uvamizi kilichofanywa na makomandoo wake kwa kuvamia nchini humo na kumuua kiongozi wa kundi la Al Qaeda, Osama Bin Laden, huku pia wakivitaka vikosi hivyo kusitisha mashambulizi ya anga katika mpaka wake na Afghanistan.

Waziri mkuu wa Pakistan Yousuf Raza Gilani akihutubia bunge la nchi hiyo katika moja ya vikao vyake
Waziri mkuu wa Pakistan Yousuf Raza Gilani akihutubia bunge la nchi hiyo katika moja ya vikao vyake REUTERS/Prime Minister's Office/Handout
Matangazo ya kibiashara

Uamuzi huo wa wabunge umekuja saa chache mara baada ya kumaliza kikao chao kilichodumu kwa zaidi ya saa kumi kilichojadili kwa kina kitendo cha uvamizi wa makomandoo wa Marekani katika ardhi ya nchi yao na kumuua Osama Bin Laden bila usalama wa taifa kufahamu kilichokuwa kinaendelea.

Wakihutubia bunge la nchi hiyo kwa nyakati tofauti mkuu wa usalama wa taifa nchini Pakistan Ahmad shuja Pasha na mkuu wa operesheni za kijeshi wamesema kuwa kwa pamoja wamekubaliana kuiandikia barua nchi ya Marekani kuionya nchi hiyo kutorudia tena kufanya uvamizi wa kijeshi bila kuzijulisha mamlaka zinazohusika na usalama nchini humo.

Katika hatua nyingine bunge la nchi hiyo pia limetishia kutoshirikiana na Marekani katika operesheni yake nchini Afghanistan kwakuwa imekuwa ikitumia mpaka wa nchi hizo mbili kupitishia vifaa vyake vya kijeshi na kuwa nchi hiyo italazimika kufunga mpaka wake na Afghanistan endapo Marekani haitaacha kufanya mashambulizi ya mara kwa mara katika mpaka wa nchi hizo.

Hatua ya bunge la nchi hiyo kuitaka Marekani kuacha mashambulizi katika moaka wa nchi hiyo na Afghanistan inatokana na ukweli kwamba vikosi vya nchi hiyo mpaka sasa vimeua zaidi ya raia 670 wasi na hatia kwa kisingizio cha kukosea shabaha ama kuwaita waliouawa ni wafuasi wa Al Qaeda bila udhibitisho.

Majuma kadhaa yaliyopita waziri mkuu wa Pakistan Syed Yousuf Raza Gilani aliwaagiza viongozi wa usalama nchini humo kuandaa taarifa kuhusiana na tukio lililofanywa na Marekani na kuiwasilisha bungeni kwaajili ya uamuzi.

Wakati wabunge wakiazimia kuiwekea vikwazo Marekani, siku ya ijumaa wapiganaji wa kundi la Taliban nchini humo walifanya shambulio la kujitoa muhanga katika kambi moja ya mafunzo ya kijeshi iliyoko katika mji wa Shabqadar kaskazini mashariki mwa nchi hiyo na kuua watu zaidi ya 80 huku wengine 147 wakijeruhiwa.

Nchi ya Marekani imekuwa ikiendesha operesheni mbalimbali nchini humo kwa lengo la kuwasambaratisha wapiganaji wa kundi la wanamgambo wa Taliban pamoja na wafuasi wa mtandao wa kigaidi duniani wa Al Qaeda ambao wamepiga kambi nchini Pakistan na Afghanistan.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.