Senegal: Matokeo ya uchaguzi wa urais yaendelea kusubirwa
Nairobi – Nchini Senegal, matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika jana yanaendelea kusuburiwa wakati huu ripoti zikisema Bassirou Diomaye Faye mgombea mkuu wa upinzani anaongoza.
Imechapishwa:
Cheza - 01:05
Faye anaongoza kwa mujibu wa matokeo ya awali yaliyotangazwa kutoka kwenye vituo mbalimbali vya kupigia kura, dhidi ya aliyekuwa Waziri Mkuu Amadou Ba, ambaye anaungwa mkono na serikali.
Washirika wa karibu wa Ba, wanasema kwa namna matokeo yalivyo wana uhakika kuwa uchaguzi huo utakwenda kwenye mzunguko wa pili.
Wafuasi wa Faye wameanza kusherehekea mapema, wakati huu kura zikiendelea kuhesabiwa na kujumuishwa, huku wagombea saba wakiongozwa na Anta Babacar Ngom, wakimpongeza kwa kuibuka mshindi .
Iwapo Faye anayeungwa mkono na Ousame Sonko, mwanasiasa wa upinzani mwenye ushawishi, aliyezuiwa kuwania urais, atathibtishwa mshindi, atakuwa na kazi kubwa ya kufanya mageuzi makubwa nchini Senegal na kuongoza vita dhidi ya rushwa na kuhakikisha kuwa anatenegeza mazingira ya kuundwa kwa ajira hasa kwa vijana.
Ba naye amekuwa akiahidi kuendeleza uongozi wa rais Macky Sall ambaye anaondoka madarakani.
Tume ya Uchaguzi inatarajiwa kumtangaza mshindi kabla siku ya Ijumaa.