Pata taarifa kuu

Mali: Kasisi wa Ujerumani Hans Joachim Lohre aachiliwa huru

Nchini Mali, Ha-Yo yuko huru. Hans Joachim Lohre, aliyepewa jina la utani la Baba Ha-Yo na jumuiya ya Wakristo ya Bamako, punguzo la jina lake la kwanza, alitekwa nyara mnamo Novemba 20 mwaka jana, huko Bamako. Alishikiliwa mateka na kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Jnim, Kundi linalodai kutetea Uislamu na Waislamu, linalohusishwa na al-Qaeda. 

Hans-Joachim Lohre, anayejulikana kama Father Ha-Yo, mnamo mwaka wa 2021.
Hans-Joachim Lohre, anayejulikana kama Father Ha-Yo, mnamo mwaka wa 2021. © YouTube/AED-ACN (capture d'écran)
Matangazo ya kibiashara

Baada ya mwaka mmoja na siku sita za kushikiliwa kwake, hatimaye ameachiliwa Jumapili asubuhi, Novemba 26. Hakuna maelezo yaliyotolewa kuhusu mazingira ya kuachiliwa kwake. Berlin wala Bamako hawajatoa taarifa rasmi kufikia sasa.

Kuachiliwa kwake kulmethibitishwa kwa RFI na chanzo cha usalama cha Mali na jamaa na marafiki wa Baba Ha-Yo huko Bamako. Jumuiya ya Wakatoliki nchini Mali imekuwa ikiomba kuachiliwa kwa Hans Joachim Lohre tangu mwaka mmoja uliopita.

Akiwa na umri wa miaka 65 na anayeishi nchini Mali kwa takriban miaka thelathini, kasisi huyu wa Ujerumani alikuwa anatoa kozi na aliishi katika Taasisi ya Mafunzo ya Kiislam na Kikristo (IFIC) huko Bamako, taasisi inayojihusisha na mazungumzo ya kidini.

Hans Joachim Lohre alitekwa nyara alipokuwa akijiandaa kushiriki misa ya Jumapili. Msalaba aliouvaa shingoni ulipatikana karibu na gari lake, karibu na taasisi alikokuwa akiishi.

Ingawa wahusika wa utekaji nyara hawakuweza kutambuliwa rasmi, vyanzo vya kidiplomasia na usalama vimethibitisha kwamba, chini ya wiki tatu baadaye, kasisi huyo wa Ujerumani alikuwa mikononi mwa Jnim, yenye mahusiano na Al-Qaeda.

Kwa miaka mingi, kundi la wanajihadi limefanya utekaji nyara katika Sahel kuwa njia ya kufadhili na kuna mateka wengi wa Mali na Magharibi ambao bado mikononi mwa kundi hili au wameshikiliwa mateka. Lakini Baba Ha-Yo alikuwa wa kwanza kutekwa nyara katikati mwa mji mkuu wa Mali.

Baada ya kuachiliwa huru amerejea nchini Ujerumani.

"Tumejawa na furaha na tunatoa shukrani," amesema mmoja wa jamaa zake, mshiriki wa jumuiya ya Kikatoliki ya Bamako na ambaye hakutaka kutajwa jina lake hadi mamlaka ya mpito ya Mali itakapotoa taarifa rasmi kuhusu kuachiliwa kwake. “Huu ni wakati wa sherehe na ahueni kwa wote waliosali na kutarajia kurejea kwake salama. Tunashukuru kwa matokeo haya ya furaha,” ameongeza.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.