Pata taarifa kuu

Somalia: Mafuriko yaua hamsini na 700,000 kutoroka makazi

Mafuriko yamesababisha vifo vya watu 50 na kusababisha karibu watu 700,000 kuyahama makazi yao nchini Somalia, afisa wa serikali ametangaza, huku mvua kubwa ikitarajiwa kuzidisha hali hiyo.

Watoto wa Kisomali waliokimbia makazi yao wakipitia maji ya mafuriko nje ya makazi yao ya muda kufuatia mvua kubwa iliyonyesha katika kambi ya Al Hidaya ya wakimbizi wa ndani, viungani mwa Mogadishu, Somalia, Novemba 6, 2023.
Watoto wa Kisomali waliokimbia makazi yao wakipitia maji ya mafuriko nje ya makazi yao ya muda kufuatia mvua kubwa iliyonyesha katika kambi ya Al Hidaya ya wakimbizi wa ndani, viungani mwa Mogadishu, Somalia, Novemba 6, 2023. REUTERS - FEISAL OMAR
Matangazo ya kibiashara

Pembe ya Afrika inakabiliwa na mvua kubwa na mafuriko yanayohusishwa na mfumo wa hali ya hewa ya El Nino ambayo imesababisha makumi ya watu kupoteza maisha na kusababisha watu wengi kuhama makazi yao, hasa nchini Somalia, ambapo mvua kubwa imeharibu madaraja na maeneo yaliyofurika makazi.

"Watu 50 wamefariki... huku watu 687,235 wakilazimika kuyahama makazi yao," Mohamud Moalim Abdullahi, mkurugenzi wa Shirika la Kukabiliana na Majanga nchini Somalia, amesema katika mkutano na waandishi wa habari. "Mvua zinazotarajiwa kunyesha kati ya Novemba 21 na 24 zinaweza kusababisha mafuriko zaidi ambayo yanaweza kusababisha vifo na uharibifu mkubwa," ameongeza.

Siku ya Jumamosi, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilisema idadi ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na mvua kubwa na mafuriko nchini Somalia "imeongezeka karibu mara mbili katika wiki moja", huku watu milioni 1.7 kwa jumla wakiathiriwa na maafa hayo. "Kwa kuongeza, barabara, madaraja na viwanja vya ndege vimeharibiwa katika mikoa kadhaa, na kuathiri usafirishaji wa watu na vifaa na kusababisha kuongezeka kwa bei za bidhaa za kimsingi," OCHA ilisema.

Shirika la misaada la Uingereza la Save the Children lilisema siku ya Alhamisi kuwa zaidi ya watu 100, wakiwemo watoto 16, wamefariki dunia na zaidi ya watu 700,000 wamelazimika kuhama makaazi yao nchini Kenya, Somalia na Ethiopia kufuatia mafuriko. Pembe ya Afrika ni moja wapo ya maeneo yaliyo hatarini zaidi na mabadiliko ya tabia nchi na hali mbaya ya hewa inazidi kuwa ya mara kwa mara na makali.

Kanda hiyo inatoka katika ukame mbaya zaidi katika miongo minne, baada ya misimu kadhaa ya mvua ya kukatisha tamaa ambayo ilisababisha mamilioni ya watu kuhitaji na kuharibu mazao na mifugo. Mashirika ya misaada yameonya kwamba hali itazidi kuwa mbaya na kutaka uingiliaji kati wa haraka wa kimataifa kwani El Nino inatarajiwa kudumu hadi angalau mwezi Aprili 2024.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.