Pata taarifa kuu

DRC: Ripoti ya ICRC yaonyesha watu 600,000 wamekimbia makazi kutokana na vita

NAIROBI – Ripoti mpya ya Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) imeonyesha kuwa watu takribani laki sita wamelazimika kukimbia makaazi yao kufuatia mapigano kati ya makundi ya wapiganaji wenye silaha, na jeshi la serikali mkoani Kivu Kaskazini, mashariki mwa DRC kwa muda wa miezi sita pekee.

Wafanyakazi wa misaada wa ICRC wa Kongo wanasaidia watu waliohamishwa makazi yao ambao wanakaribia kupokea msaada wa chakula, huko Kibati, Novemba 5, 2008.
Wafanyakazi wa misaada wa ICRC wa Kongo wanasaidia watu waliohamishwa makazi yao ambao wanakaribia kupokea msaada wa chakula, huko Kibati, Novemba 5, 2008. AFP/Yasuyoshi Chiba
Matangazo ya kibiashara

Katika taarifa yake kwa Vyombo vya habari iliyochapishwa Agosti 10, Kamati hiyo ya ICRC, imesema asilimia 18 ya watu walioyahama makazi yao wanaishi katika viunga vya mji wa Goma katika makanisana shule.

ICRC imeendelea kusema kuwa asilimia 82 wanaishi katika familia zilizowapokea, na kwamba wengi wao hawana msaada wowote.

Kamati hiyo ya Msalaba mwekundu pia imesema kuongezeka kwa ukosefu wa usalama kunatatiza utoaji wa misaada katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi na vurugu, na kwamba kwa muda wa miezi sita pekee watu kama laki sita kukimbia makwao, ni idadi kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika Ulimwengu.

Mbali na Goma, ripoti hiyo imeonyesha kuwa wakazi wachache waliobaki kwenye mji wa Oicha, wenye wakazi laki tatu na sitini  kaskazini mwa jiji la Beni, wanakabiliwa na ukosefu wa usalama.

Wakaazi hao wamekuwa wakikabiliwa na mashambulio yanayohusishwa na ADF ambao wamekuwa wakisakwa na majeshi ya FARDC ambayo yanashirikiana na jeshi la Uganda UPDF, hali ambayo pia imesababisha baadhi ya raia kukimbia nyumba zao na kuelekea mjini Beni.

Anne-Sylvie Linder, mkuu wa wajumbe wa ICRC mjini Goma, amewataka wafadhili kuendelea kusaidia makundi mbalimbali ya kibinadamu ambayo yanafanya kazi katika eneo hilo, katika kuhakikisha misaada ya kibinadamu inawafikia wanaohitaji licha ya kwamba mashirika ya kibinadamu yanakabiliwa na ukosefu wa ufadhili na vikwazo vya kufikia jamii zinazohitaji msaada.

Ripoti imeandaliwa na Ruben Lukumbuka.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.