Pata taarifa kuu

Magonjwa yasiyo ya kuambukiza bado ni tishio barani Afrika.

NAIROBI – Muungano wa taasisi za magongwa yasiyo ya kuambukiza nchini Kenya, NCDAK, umezindua mpango wa kimkakati wa miaka mitano, wa kuhakikisha muungano huo unajituma ili kutimiza maono yake ya nchi ya Kenya ambayo haina magonjwa yasiyo ya kuambukiza, maarufu NCD-free Kenya.

Ugonjwa wa kisukari ni mojawapo ya aina ya magonjwa yasio ya kuambukiza
Ugonjwa wa kisukari ni mojawapo ya aina ya magonjwa yasio ya kuambukiza AFP/Archivos
Matangazo ya kibiashara

Mkurugenzi mkuu wa muungano huo Dr. Catherine Karekezi, amesema huduma za kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza zinapaswa kupewa kipau mbele ili kufikia malengo la kimataifa.

“Watu wanaoishi na magonjwa ya NCD waliathirika na janga la Uviko 19. Janga hili limefichua ukosefu wa usawa na udhaifu wa mifumo ya afya haswa katika mataifa yanayoendelea kukiwemo nchi ya Kenya,” Amesema Karekezi.

Mpango huu wa kuanzia mwaka 2023-2027, una lengo la kukabiliana na janga la magonjwa yasiyo ya kuambukiza, kuafikia malengo ya maendeleo endelevu ya mwaka 2030 ulimwenguni na vilevile kutimiza ajenda ya Vision 2030 nchini Kenya.

Katika mpango huu, muungano huo utatumia nguzo za utetezi, kuwashirikisha watu wanaoishi na magonjwa yasiyo ya kuambukiza pamoja na utafiti na usimamizi wa maarifa ikizingatiwa kuwa nchini Kenya, takwimu ni chache za kuaminika kuhusu NCD ambazo zitasaidia katika utetezi na kubuni sera.

Kwa mujibu wa shirika la afya duniani, WHO, magonjwa ya NCD, yanasabisha asilimia 74 ya vifo kote ulimwenguni na nyingi ya vifo vinatokea katika nchi zinazoendelea, kutokana na wagonjwa kutofikia huduma za kinga na za kudhibiti magonjwa hayo.

Nchini Kenya, magonjwa yasiyo ya kuambukiza, yanasababisha asilimia 41 ya vifo, pia yana athari kwa mtu binafsi na familia kutokana na kupoteza tija na gharama ya juu ya kukabiliana na magonjwa haya.

Magonjwa ya NCD yanajumuisha saratani, magonjwa ya moyo, kisukari, magonjwa ya mapafu, matatizo ya afya ya akili, miongoni mwa mengine.

Katika ripoti yake ya kila mwaka ya mwaka 2022, muungano wa NCDAK, umesema ulifanikiwa kuwapa mafunzo wahudumu wa afya 102 na watu 50 wanaoishi na saratani ya mapafu, huku zaidi ya watu elfu thelathini wakihamasishwa kuhusu ugonjwa huu. Awamu ya pili itafanyika mwezi huu wa Juni.

Jupiter Mayaka- RFI Kiswahili

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.