Pata taarifa kuu

HRW: Mauaji ya kikabila yanaendelea kushuhudiwa magharibi mwa Tigray

NAIROBI – Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Human Rights Watch katika ripoti yake ya hivi punde, limetuhumu mamlaka eneo la Tigray pamoja na vikosi vya Amhara kwa kutekeleza mauaji ya kikabila magharibi mwa jimbo la Tigray nchini Ethiopia.

Wakimbizi wa Ethiopia, wanaokimbia mapigano katika eneo la Tigray kaskazini mwa nchi hiyo, wanavuka mpaka na kuingia Hamdayet, Sudan, 13 Novemba 2020.
Wakimbizi wa Ethiopia, wanaokimbia mapigano katika eneo la Tigray kaskazini mwa nchi hiyo, wanavuka mpaka na kuingia Hamdayet, Sudan, 13 Novemba 2020. © UNHCR/Hazim Elhag
Matangazo ya kibiashara

Ripoti ya shirika la Human Rights Watch inasema tangu mkataba wa amani wa Novemba mwaka uliopita, mamlaka katika eneo hilo pamoja na vikosi vya Amhara vimeendelea kutekeleza mauaji kwa misingi ya kikabila.

HRW, imeitaka serikali ya Ethiopia kuwachukulia hatua wote wanaohusika katika vitendo hivyo.

Ripoti hiyo pia imeangazia namna mamlaka zimekiuka haki za raia wa eneo hilo, ikiwemo kufanya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu. Makanali Demeke Zewdu na Belay Ayalew, wametajwa kuhusika pakubwa katika ukiukaji huo.

Ripoti hiyo pia inataka serikali ya Ethiopia kuruhusu uchunguzi huru kufanyika iwapo kweli ina nia ya kuhakikisha haki inapatikana kwa waathiriwa katika jimbo la Tigray, mkurugenzi wa shirika hilo katika pembe ya Afrika, Laetitia Bader akisema raia waliosalia katika eneo hilo wako katika hatari.

Wengi wa wale ambao wameuawa  eneo hilo, walikuwa wafungwa, na waliuawa hata baada ya kufungwa kwa zaidi ya mwaka moja jela, haya yote ni kutokana na hali kwamba wao ni raia   wa Tigray. Ni wazi kwamba hadi kufikia sasa hapajakuwa na uchuguzi wowote kwa vitendo hivi eneo la magharibi mwa Tigray, na raia wanaosalia eneo hilo wapo katika hatari. Amesema Bader.

 

Kwa sasa kuna ujumbe wa Umoja wa Afrika unaofuatilia hali kule Tigray, na unatarajiwa kuweka wazi ripoti yake kuhusu hali ya kibidanamu jimboni humo.

Miaka miwili iliyopita serikali ya Ethiopia na wapiganaji wa TPLF, walikubaliana kusitisha mapigano yaliyodumu kwa miaka miwili na kusababisha maelfu ya raia kuuawa huku wengine wakikimbia makwao.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.