Umoja wa mataifa umeongeza muda wa vikwazo kwa Sudan Kusini
NAIROBI – Baraza la usalama katika umoja wa mataifa limeongeza muda wa vikwazo vilivyoekewa Sudan Kusini kuhusu silaha kwa kipindi cha mwaka mmoja zaidi, baadhi ya watu binafasi nchini humo pia wakiwa wameekwa vikwazo vya usafiri na mali zao kuzuiwa.
Imechapishwa:
Baraza hilo lilipiga kura siku ya Jumanne ya wiki hii, kura kumi zikipigwa kuidhinisha hatua hiyo, wanachama wengine watano wakikosa kupiga kura.
Katika uamuzi wake, baraza hilo limezitaka nchi wanachama wa umoja wa mataifa kuzuia uuzaji wa moja kwa moja wa silaha au usafirishaji wa silaha kupitia nchi nyengine kwa taifa hilo la Sudan Kusini.
Vikwazo vya silaha viliongezwa hadi Mei mwaka ujao, huku baraza hilo likielezea wasiwasi wake juu ya kuendelea kuongezeka kwa ghasia na mzozo wa kisiasa wa muda mrefu.
Hali mbaya ya kiusalama, kiuchumi na na hali ya kibinadamu katika maeneo mengi ya nchi hiyo pia ikielezwa kuwa mbaya. Nchi zilizosusia ni China, Russia, Ghana, Gabon na Msumbiji.
Balozi Akuei Bona Malwal kutoka Sudan Kusini amekashifu hatua hiyo akisema "ilifanyika kwa nia mbaya ikiwa na malengo mabaya
Licha ya makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mwaka 2018, ghasia zinaendelea na hadi kufikia Aprili mwaka huu watu milioni 2.3 nchini Sudan Kusini wamethibitishwa kuwa wakimbizi wa ndani.