Pata taarifa kuu

Sudan inataka kutimuliwa kwa mwakilishi wa UN Volker Perthes

NAIROBI – Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anasema "ameshangazwa" na barua kutoka kwa mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan, inayoripotiwa kuomba kubadilishwa kwa mjumbe maalum wa UN nchini Sudan Volker Perthes wakati huu kukiwa na mapigano nchini humo kati ya Jeshi na wanamgambo wa RSF.

 Volker Perthes, Mkuu wa UN nchini Sudan
Volker Perthes, Mkuu wa UN nchini Sudan AFP - -
Matangazo ya kibiashara

Kupitia kwa taarifa ya msemaji wa umoja wa mataifa Stephane Dujarric, Guterres ameeleza kuwa anajivunia kazi iliyofanywa na Volker Perthes ambapo pia ana imani na mjumbe wake maalum nchini Sudan.

Taarifa ya UN inakuja wakati huu makabiliano yakiwa yanaendelea nchini Sudan kati ya vikosi vya serikali chini ya uongozi wa jenerali Al-Burhan na naibu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo anayeongoza wapiganaji wa RSF.

Mapigano yameripotiwa katika baadhi ya maeneo ya Sudan hata wakati huu ambapo mazungumzo yanayolenga kupata muafaka kati ya pande hizo mbili hasimu yakiingia siku yake ya tano.

Makabiliano kati ya wanajeshi wa Sudan na wapiganaji wa RSF yamendelea kuripotiwa nchini humo licha ya kuwepo kwa makubaliano ya kusitisha vita
Makabiliano kati ya wanajeshi wa Sudan na wapiganaji wa RSF yamendelea kuripotiwa nchini humo licha ya kuwepo kwa makubaliano ya kusitisha vita © AFP

Mazungumzo hayo yanafanyika chini ya uongozi wa Marekani na Saudi Arabia, pande hizo mbili zinazopigana zikiripotiwa kuendelea kutuhumiana kwa kuvunjika kwa makubaliano ya kusitisha vita.

Umoja wa mataifa wala jeshi la Sudan hawajaweka wazi barua hiyo inayodaiwa kutumwa kwa katibu mkuu wa UN na jenerali Burhan inayotaka kuondolewa kwa Perthes kama mwakilishi wa Guterres nchini  Sudan.

Hii ni hatua ya hivi karibuni kuchukuliwa na Burhan, ambaye wiki jana alimfuta kazi rasimi Daglo kama naibu wake. Mapigano nchini Sudan yamesababisha vifo vya karibia watu 1,800 kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na mashirika ya kufuatilia mizozo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.