Pata taarifa kuu
SIASA-HAKI

Rais wa Tunisia na serikali yake washitakiwa mbele ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu

Familia za wafuasi wa upinzani nchini Tunisia waliokamatwa wamewasilisha malalamiko yao siku ya Jumatano kwenye Mahakama ya Afrika ya Haki za Kibinadamu na kudai kuachiliwa mara moja kwa ndugu zao.

Kiongozi wa chama cha Ennahdha nchini Tunisia Rached Ghannouchi, Februari 21, 2023 mjini Tunis.
Kiongozi wa chama cha Ennahdha nchini Tunisia Rached Ghannouchi, Februari 21, 2023 mjini Tunis. AFP - FETHI BELAID
Matangazo ya kibiashara

Tangu mwanzoni mwa mwezi Februari, mamlaka ya Tunisia imewafunga zaidi ya wapinzani na maafisa 20 wakiwemo mawaziri wa zamani, ukandamizaji uliolaaniwa na jumuiya ya kimataifa na mashirika ya kutetea haki za binadamu.

Rached Ghannouchi, spika wa zamani wa bunge na mmoja wa wapinzani wakuu wa Rais wa Tunisia Kais Saied, ambaye alivunja bunge Julai 2021 na kutwaa mamlaka kamili, ni miongoni mwa waliozuiliwa.

Bw. Ghannouchi, 81, kiongozi wa chama cha kihafidhina Ennahdha, alikamatwa mwezi Aprili na kuhukumiwa Mei 15 hadi mwaka mmoja jela kwa "kuunga mkono ugaidi".

Kwa mujibu wa binti yake, Yousra Ghannouchi, 45, ambaye anaishi Uingereza, mashtaka dhidi ya spika wa zamani wa bunge la Tunisia "yanachochewa kisiasa na ni uzushi" na ni sehemu ya jaribio la Bw Saied "kuondoa upinzani," ameliambia shirika la habari la AFP.

Kais Saied kwa upande wake alidai kuwa waliozuiliwa walikuwa "magaidi" waliohusika katika "njama dhidi ya usalama wa serikali".

Kukamatwa na kutiwa hatiani kumetajwa na wapinzani kama "mapinduzi" na kurejea kwa utawala wa kiimla katika demokrasia pekee iliyoibuka kufuatia machafuko katika nchi kadha za Kiarabu zaidi ya muongo mmoja uliopita.

'Hatutanyamaza'

Ndugu wa Bw Ghannouchi na wapinzani wengine kadhaa waliofungwa wamewasilisha malalamishi katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Kibinadamu mjini Arusha, Tanzania, kama sehemu ya kampeni ya kimataifa ya kutaka waachiliwe.

"Tunatumai hii itawezesha kuachiliwa kwao na kupata haki," Yousra Ghannouchi amsema mjini Nairobi siku ya Jumanne, mkesha wa safari ya Arusha.

"Hawajanyamaza na hatutanyamaza," ameongeza.

Yousra Ghannouchi, kama ndugu wengine kadhaa wa wafungwa, pia ametoa wito kwa Marekani, Umoja wa Ulaya na Uingereza kuweka vikwazo dhidi ya Bw. Saied na mawaziri kadhaa ambao "wote wanahusishwa na ukiukaji wa haki za binadamu".

"Wanajaribu kutetea kesi zao nchini Tunisia lakini milango yote imefungwa," Rodney Dixon, wakili wa Bw. Ghannouchi na watu wengine watano waliofungwa, ameliambia shirika la habari la AFP.

Bw Dixon amesema jamaa hao walitaka kuchukua hatua za kisheria ili kubaini kuwa vifungo hivyo ni kinyume na sheria ya haki za binadamu ya Afrika na kuwawezesha kuachiliwa.

"Hakuna haki kupitia mfumo huko (...), ndiyo maana wanapaswa kufika" mbele ya Mahakama ya Afrika, amesema Bw. Dixon, akiongeza kuwa wafungwa hawakuwa na mawakili wa mara kwa mara na walishindwa kupata huduma za matibabu zinazofaa.

Wakili huyo pia amesema "tuhuma ya utesaji" kuhusu mfungwa itawasilishwa mahakamani.

Yousra Ghannouchi amesema ana wasiwasi kuhusu afya ya babake kwani anaugua shinikizo la damu na "si kijana tena".

Spika huyo wa zamani wa Bunge alifungwa mara mbili katika miaka ya 1980 kwa shughuli za kisiasa za siri kabla ya kwenda uhamishoni kwa miaka 20 na kisha kurejea baada ya kupinduliwa kwa dikteta Zine El Abidine Ben Ali mwaka 2011.

Tunisia ni mojawapo ya nchi sita barani humo ambazo zimejiunga kikamilifu na Mahakama ya Afrika ya Haki za Kibinadamu na Watu.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.