Sudan: Tutatekeleza mkataba wa usitishaji mapigano: Kiongozi wa RSF
NAIROBI – Kiongozi wa kundi la wapiganaji wenye nguvu nchini Sudan la RSF, Mohamed Dagalo, akisema wapiganaji wake watatekeleza mkataba wa usitishaji mapigano ulioanza kufanya kazi hapo jana baada ya kutiwa saini mwishoni mwa juma mjini Jeddah, Saudi Arabia.
Imechapishwa:
Baada ya kuzuka hofu kuhusu mahali aliko tangu kuanza kwa vita hiyo mwezi uliopita, Dagalo kupitia rekodi ya sauti, amezipongeza jumuiya za kikanda na hasa Saudi Arabia, kwa kusimama imara kutafuta suluhu ya mzozo unaoendelea kati yake na Jenerali, Abdel Fattah al Burhani.
Kauli yake imekuja siku chache kupita tangu afutwe kazi na Burhani kama naibu wake, ambapo pia akaunti za benki za kundi lake zimezuiliwa, kitendo ambacho mwenyewe amekikashifu.
"Tutaendelea kuwajibika kwa usalama wa nchi yetu na sisi tunaamini vita hivi vililazimishwa kwetu pia tutawaajibisha watu waliohusika na mapinduzi pamoja na washirika wao ambapo walipindua na kupindisha njia ya demokrasia ambayo Sudan ilikuwa inaelekea." alisema Mohamed Dagalo.
Mohamed Dagalo, Kiongozi wa RSF nchini Sudan
Licha ya kuaanza kutekelezwa kwa mkataba wa usitishaji wa vita nchini Sudan hapo Jumatatu ya wiki hii, kumeendelea kuripotiwa makabiliano kwenye mji wa Khartoum, kati ya vikosi hasimu.
Kwa mujibu wa raia walioko kwenye mji huo, milio ya risasi na roketi imesikika usiku kucha, huku baadhi hata wakichapisha picha za video kupitia kwenye mitandao ya kijamii, zikionesha moshi ukiwa umetanda kwenye maeneo mengi.
Hali kala hii pia imeripotiwa kwenye miji ya Omdurman na Bahri, ambapo nako mashuhuda wameripoti uwepo wa makabiliano.
Baada ya wiki tano za mapigano kati ya jeshi la Serikali na vikosi vya RSF, pande hizo mwishoni mwa juma lililopita zilitiliana saini mkataba wa usitishaji vita kwa siku 7 kuanzia jana, ili kuruhusu misaada ya kibinadamu kuwafikia mamia ya raia walionaswa kwenye mapigano.
Kumekuwa na wasiwasi ikiwa makubaliano haya yatadumu, hasa ikizingatiwa kuwa saa chache kabla ya utekelezwaji wake hapo jana, jeshi lilifanya mashambulio ya anga kulenga ngome za RSF, huku kundi hilo likijibu hata baada ya muda wa makataa hayo kuanza.
Makubaliano haya yameamsha tena matumaini ya vita kukoma, vita ambayo hadi sasa imesababisha raia zaidi ya milioni 1 na laki 1 kukimbia nyumba zao, wakiwemo laki 2 na elfu 50 waliokimbilia nchi jirani.