Pata taarifa kuu

Kenya na Somalia zakubaliana kufungua mpaka wao uliofungwa kwa zaidi ya miaka 10

Nairobi – Kenya na Somalia zimekubaliana kufunguliwa  kwa awamu kwa mpaka wao wa pamoja baada ya zaidi ya mwongo mmoja, waziri wa mambo ya ndani wa Kenya Kithure Kindiki  amesema hii leo wakati uhusiano kati ya majirani hao wawili ukiongezeka kufuatia mvutano wa miaka mingi.

Waziri wa Usalama wa ndani wa Somalia,Dr. Mohamed Ahmed Sheikh Ali na mwenzake wa Kenya Dr. Kithure Kindiki
Waziri wa Usalama wa ndani wa Somalia,Dr. Mohamed Ahmed Sheikh Ali na mwenzake wa Kenya Dr. Kithure Kindiki © Handout
Matangazo ya kibiashara

Tangazo hilo lilitolewa baada ya mkutano wa ngazi ya juu wa mawaziri mjini Nairobi kuhusu ushirikiano ikiwa ni pamoja na masuala ya usalama, pamoja na biashara na ongezeko la watu.

Mpaka huo ulikuwa umefungwa rasmi mwaka wa 2011 kwa sababu ya mashambulizi katika ardhi ya Kenya na kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Al-Shabaab la Somalia.

 "Tumeazimia kwamba mpaka kati ya Kenya na Somalia utafunguliwa kwa awamu ndani ya siku 90 zijazo, kuanzia leo," Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki alisema, akiongeza kuwa kivuko cha kwanza kinafaa kufunguliwa baada ya siku 30.

Mataifa hayo mawili yalikuwa yametangaza mipango Julai mwaka jana ya kufungua tena mipaka katika mazungumzo kati ya rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud lakini hayakutimia.

Kindiki alisema watafanya kazi pamoja kuhusu usalama, kuboresha upashanaji habari na taratibu za ushirikiano wa kuvuka mpaka.

 "Kenya na Somalia zinaendelea kukabiliwa na changamoto za usalama wa ndani na zinazotokana na kundi la Al-Shabaab," aliongeza.

Kenya ni mchangiaji mkubwa wa wanajeshi katika operesheni ya kijeshi ya Umoja wa Afrika dhidi ya Al-Shabaab yenye mafungamano na  kundi la Al-Qaeda, ambayo imekuwa ikiendesha uasi nchini Somalia kwa zaidi ya miaka 15.

Uhusiano kati ya mataifa hayo mawili umekumbwa na mzozo wa mpaka wa baharini pamoja na shutuma za Wasomali kwa Wakenya kuingilia masuala yake, huku Nairobi ikiishutumu Mogadishu kwa kuitumia kama mbuzi wa kuachilia matatizo yake ya kisiasa na kiusalama.

Somalia ilikata uhusiano wa kidiplomasia mnamo Desemba 2020 baada ya Nairobi kuwa mwenyeji wa uongozi wa kisiasa wa Somaliland, eneo lililojitenga lisilotambuliwa na serikali kuu huko Mogadishu.

Kenya na Somalia zina mpaka wa nchi kavu wenye urefu wa kilomita 680 (maili 420) na zimekuwa kwenye mzozo wa muda mrefu kwa miaka mingi kuhusu eneo linaloweza kuwa na utajiri wa mafuta na gesi katika Bahari ya Hindi.

Mnamo Oktoba 2021, mahakama kuu ya Umoja wa Mataifa ilikabidhi udhibiti wa sehemu kubwa ya eneo hilo kwa Somalia lakini Kenya ilikataa uamuzi huo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.