Pata taarifa kuu

Cyril Ramaphosa atoa wito wa kukomesha mzozo mashariki mwa DRC

NAIROBI – Rais wa Afrika Kusini, ametuhumu makundi ya waasi yanayoendeleza mashambulizi mashariki mwa DRC, na kutaka makundi hayo pamoja na wale wanayoyafadhili kukoma mara moja vitendo hivyo.

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa
Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa © ©CyrilRamaphosa
Matangazo ya kibiashara

Rais Cyril Ramamphosa amesema Afrika Kusini iko tayari kuchangia kwa vyovyote ili kupatikana kwa amani mashariki mwa DRC.

Afrika Kusini iko tayari kuchangia katika uundaji wa vyombo madhubuti vya kikanda ambavyo vinaweza kusaidia kuleta utulivu na amani mashariki mwa DRC. Kwa hiyo tunaunga mkono haja ya mipango ya muda mrefu chini ya SADC.

Mchambuzi wa masuala ya siasa John Shabani, kutoka Goma, nchini DRC, ameelezea maana ya kauli hii ya Ramaphosa, ikizingatiwa wanajeshi wa Afrika Kusini tayari wanahudumu chini ya kikosi cha MONUSCO nchini DRC.

Nini ambayo hawakufanya ndani ya MONUSCO ambayo wanakuja kufanya wakija wao wenyewe? Ndio maana Wakongomani wanaona ni kama wana ajenda nyingine, kitu ambacho wanataka kufanya wangefanya miaka 25 iliyopita, Amesema Shabani.

Mkutano wa SADC, Namibia

Katika mkutano wa mapema wiki hii nchini Namibia, uliowaleta pamoja viongozi kutoka nchi wanachama wa SADC, mbali na viongozi hao kupokea ripoti ya kutathmini hali ilivyo DRC, Ramaphosa alilaani makundi yanayoyumbisha usalama katika eneo hilo.

Marais wa nchi wanachama wa Muungano wa SADC, Mei 8, nchini Namibia.
Marais wa nchi wanachama wa Muungano wa SADC, Mei 8, nchini Namibia. © @SADC_News

 

Kwa mujibu wa shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa, mzozo kati ya makundi ya kujihami na majeshi ya serikali, yamesababisha zaidi ya watu laki nane kuyahama makwao tangu mwezi Machi 2022.

Wito wa Tshisekedi

Jumanne wiki hii, rais wa DRC Félix Tshisekedi, alisema kuwa kikosi cha EAC huenda kikaondoka nchini humo kufikia Juni mwaka huu, iwapo halitafanikiwa katika majukumu yake mashariki mwa nchi hiyo.

Majukumu ya EACRF yanakamilika mwezi Juni, ikiwa kufikia wakati huo tutatathmini kwamba jukumu lao halijatekelezwa, tutawarudisha wanajeshi hao nyumbani kwa heshima na kuwashukuru kwa kujaribu kuleta mchango wao katika kuleta amani nchini DRC.

Akiwa ziarani nchini Botswana, Tshisekedi ameunga mkono mpango wa muungano wa SADC, kutuma vikosi vyake nchini mwake.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.